Wednesday, February 11, 2009

Taifa Stars, Zimbabwe Nguvu Sawa

HUKU zikijiandaa kwa fainali za Afrika za wachezaji wa ligi za ndani, CHAN, timu ya Taifa Stars na wageni wao, Zimbabwe zimeshindwa kukonga nyoyo za mashabiki wengi waliofurika Uwanja wa zamani wa Taifa, Dar es Salaam na kutoka suluhu.

Katika mchezo huo ambao ulishuhudiwa na maelfu ya mashabiki wengi wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete aliyeingia uwanjani hapo kushuhudia , yeye ndiye aliyeshangiliwa zaidi.

Hata hivyo, kwa kiasi kikubwa cha kipindi cha kwanza, pia kile cha pili, mchezo huo ulionyesha kupooza kwa kukosa kasi ya kuridhisha.

Stars, kwa upande wao ndio walioanza kulikaribia lango la Wazimbabwe, wakianza kutia matumaini kwa mashabiki wao tangu dakika ya tatu ya mchezo, kisha tena dakika ya tano na saba kuwa wangeibuka na ushindi, lakini walijikuta wakikosa mbinu za kuweza kukwamisha mipira wavuni.

Baadhi ya mipira ya kona katika muda huo, ama ilikosa waunganishaji au mingine ikiokolewa na kipa wa Zimbabwe, Willard Nyamatera aliyepangua shuti kali la dakika ya 12, la beki Shadrack Nsajigwa.

Phillip Marufu wa Zimbabwe, alimjaribu kipa Shaaban Dihile kwa shuti, dakika ya 13, lakini kipa huyo alikaa chonjo na kulidaka.

Stars ilipata pigo dakika ya 22 baada ya kiungo wake, Nizar Khalfan kuumia na kutoka nje na nafasi yake kuchukuliwa na Mwinyi Kazimoto.

Katika mchezo huo, mabeki wa Zimbabwe walimkamia na kumchezea rafu, kumkwatua mshambuliaji Mrisho Ngassa. Jaribio la dakika ya 25 la Haruna Moshi ambaye aliachia mkwaju mkali, lilizimwa tena na kipa wa Zimbabwe.

Ukosefu huo wa umakini uliendelea kuwasumbua wachezaji wa Stars huku kiungo mgeni, Kazimoto akiungana na Jerry Tegete katika kukosa nafasi nzuri ya kufunga bao, dakika ya 40.

Kwa upande wao, mashabiki nao walisikika wakipiga kelele za kumtaka kocha, Marcio Maximo ampumzishe Tegete kutokana na kupooza kwa kiasi kikubwa katika mchezo huo.

Kipindi cha pili, Maximo aliwapumzisha Tegete, Kazimoto na kuwaingiza Mussa Hassan Mgosi na Kigi Makassi huku Zimbabwe pia ikifanya mabadiliko kadhaa katika kikosi chake, ambayo hata hivyo hayakusaidia kubadili mchezo huo ambao uliendelea kupooza.

Mashambulizi mengi ya Stars langoni mwa Zimbabwe ambayo hayakuwa na malengo yalizimwa na mabeki wa Zimbabwe na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa suluhu 0-0.

Kocha wa Zimbabwe, Sunday Marimo alieleza baada ya mchezo huo kuwa vijana wake walijitahidi kucheza vizuri na kueleza kuwa Stars wameonyesha kiwango cha kuridhisha, lakini mchezo ulikuwa mgumu. Marimo alieleza kutiwa moyo na timu zote mbili kuwa zitakwenda Ivory Coast zikiwa zimekamilika.

Kocha huyo alikuwa kivutio baada ya filimbi ya mwisho alipowaita wachezaji wa pande zote mbili na kuwapa mazoezi ya viungo.

Maximo aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza vizuri katika mchezo huo uliokuwa mgumu kutokana na aina ya uchezaji wa wapinzani wao walioweka viungo wengi zaidi na kuwanyima nafasi ya kupenya na kucheza mchezo wao wa kawaida.


No comments:

Post a Comment