WATANZANIA wana raha robo tu katika michuano inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika baada ya Yanga kuibuka timu pekee katika michezo ya mwanzo hatua ya awali, kwa kuitandika Etoile d’Or ya Comoro mabao 8-1.
Katika hali ya huzuni, timu nyingine tatu zimejikuta zikipata matokeo ya vipigo, hali inayoleta huzuni, kwani katika timu nne, ni Yanga inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika iliyoanza vizuri, tena kwa kishindo.
Lakini wawakilishi wengine katika michuano hiyo, Miembeni kutoka Zanzibar ilijikuta ikilambwa mabao 2-0 na Monomotapa ya Zimbabwe katika mchezo uliofanyika mjini Harare.
Katika michuano ya kuwania Kombe la Shirikisho (CAF), Tanzania Prisons ilibanjuliwa nyumbani jana na Khalij Sert ya Libya katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kipigo hicho kimekuja siku moja baada ya wawakilishi wengine kwenye michuano hiyo, Mundu ya Zanzibar kupigwa mabao 6-0 na Red Arrows ya Zambia, katika mchezo uliofanyika mjini Lusaka juzi.
Katika mchezo jana Tanzania Prisons walianza kuwa wanyonge mapema baada ya winga machachari wa Khalij, Abdullah Shaiji kupiga bao la kuongoza.
Nyota huyo, aliyeonekana kuwa nyota wa mchezo alifunga bao hilo katika dakika ya pili, baada ya kuwatoka mabeki wa Prisons na kupiga shuti na kipa wa timu hiyo, Exevery Mapunda, kuutema na kuumalizia tena kwa kisigino.
Prisons ambayo licha ya kufungwa ilitandaza soka safi katika kipindi cha pili cha mchezo huo na wachezaji wakongwe wa timu hiyo Yona Ndabila na Henry kukosa nafasi nyingi ambazo kama wangezitumia vyema, wangefunga.
Khalij ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao moja. Wakati timu zinaingia kipindi cha pili, mabeki wa Prisons walipata kibarua kigumu baada ya winga wa kushoto Masuud Ghinai kuwachosha, kutokana na kupiga chenga huku akiwa anakimbia.
Katika dakika ya 62, mshambuliaji wa kutegemewa wa Khalij, Saadulah Wafidia aliwanyanyua mashabiki na wapenzi wa timu hiyo ambao ni raia wa Libya waliojitokeza kuishangilia, baada ya kufunga bao la pili, alipopokea krosi safi kutoka kwa Dibati Musa.
Hadi kipenga cha mwisho cha Alfred Ndinya kinapulizwa, matokeo ya mchezo huo yalikuwa ni 2-0, kwa matokeo hayo Prisons itakuwa na kibarua kigumu cha kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Libya wiki mbili zijazo, kama ilivyo kwa timu nyingine za Tanzania, isipokuwa Yanga.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Prisons, James Nestory, alisema papara za washambuliaji wake zimechangia kwa kiasi kikubwa kwa kuwachosha mabeki na viungo wa timu hiyo.
No comments:
Post a Comment