Monday, February 16, 2009

Prisons yaendeleza uteja Libya

Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kuwania kombe la Shirikisho timu ya Prisons, imetupwa nje ya michuano hiyo kwa jumla ya bao 6-0, baada ya juzi kukubali kichapo cha bao 4-0 kutoka kwa wapinzani wao Khalij Sert ya Libya.

Katika mchezo huo uliochezwa Tripol, Prisons ilitakiwa kushinda bao 3-0,ili iweze kusonga mbele kutokana na kukubali kichapo cha bao 2-0, katika mchezo wa awali uliochezwa kwenye uwanja wa Uhuru zamani uwanja wa taifa, jijini Dar es Salaam.

Prisons, ilionekana thaifu mbele ya Khalij Sert kutokana na kucheza hovyo katika dakika zote za mchezo, ambapo iliwachukua muda mfupi walibya hao kupachika bao la kuongoza.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka Libya zimeeleza kuwa wawakilishi hao wa Tanzania walishindwa kufurukuta mbele ya khalij, ambapo hawakufanya hata shambulizi la maana langoni mwa wapinzani wao.

Kwa matokeo hayo Prisons itakuwa imeungana na wawakilishi wengine wa Zanzibar kutolewa kwenye michuano ya kimataifa,ambazo ni timu ya Miembeni na Mundu, ambapo Miembeni imetolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Monomotapa ya Zimbabwe kwa jumla ya bao 3-2.

Mundu imetolewa na Red Arrows ya Zambia kwa jumla ya bao 7-0, baada ya kukubali kichapo cha bao 6-0,kwenye mchezo wa awali na katika mchezo wa marudiano uliochezwa jijini Dar es salaam timu hiyo ilifungwa bao 1-0.

Hiyo ni mara ya tatu kwa Prisons kushindwa kufanya vizuri kwenye michuaano ya kimataifa kutokana na kutolewa katika hatua za awali katika miaka yote iliyowahi kushiriki.

Timu hiyo inatarajia kurejea jijini Dar es Salaam keshokutwa na mara baada ya kutua jijini itakaa kwa muda mfupi kabla ya kurejea Mbeya kuendelea na maandalizi ya raundi ya pili ya Ligi Kuu.




Source: Nipashe

No comments:

Post a Comment