Sunday, February 1, 2009

Rais Mpya achaguliwa Somalia

Sheikh Sharif Ahmed , Rais mpya wa Somalia

Kiongozi anayefuata msimamo wa wastani wa WaIslamu, Sheikh Sharif Ahmed amechaguliwa kuwa rais mpya wa Somalia, baada ya kura ya siri ya wabunge wa Somalia.

Bwana Ahmed alishinda kwa kura za kutosha katika duru ya pili ya upigaji kura, baada ya mshindani mwenzake mmoja, Waziri Mkuu Nur Hassan Hussein kujitoa katika mashindano.

Bwana Ahmed amechaguliwa na bunge baada ya Rais Abdullahi Yusuf Ahmed kujiuzulu.

Wabunge walikutana Djibouti kwa vile hakuna utulivu Somalia, ambako wapiganaji Waislamu wanadhibiti sehemu kubwa ya nchi.

Bwana Ahmed alikuwa kiongozi wa upinzani ambao ukishutumiwa kuwa na mshikamano na Al Qaeda. Mwandishi wa BBC katika eneo hilo, Peter Greste, anasema Bwana Ahmed alishinda uchaguzi, kwa sababu anaonekana anaweza kushirikiana na pande mbili tofauti za wababe wa kivita, ambao hadi sasa wamekuwa wakiidhibiti serikali na wapiganaji wa Al-Shabab.

Mapema juma hili, wanachama wapya 149 kutoka upande wa upinzani wa Muungano wa Kuikomboa tena Somalia, ambao wanaongozwa na Bwana Ahmed, waliapishwa na kuwa wabunge.

Lakini Al-Shabab inasema kuwa haitoitambua serikali mpya; serikali ambayo inatarajiwa kuhama kutoka Djibouti hadi mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, katika siku chache zijazo.

Lakini Mogadishu inakabiliwa na fujo, na hakuna askari wa kutosha wa kuweka amani kutoka Umoja wa Afrika, kuweza kuwalinda wabunge. Inafikiriwa kuwa baadhi yao watabaki Djibouti na wengine watakwenda Kenya.

Wapiganaji wa Al-Shabab wanadhibiti mji wa Baidoa, ambako bunge zamani likikutana, pamoja na maeneo kadha ya kati na kusini mwa Somalia.


Source: BBC

No comments:

Post a Comment