Monday, February 16, 2009

Ngassa awachachafya Wacomoro

Winga nyota Mrisho Ngassa jana aling'ara wakati alipopachika mabao manne wakati Yanga ilipoibuka na ushindi wa 6-0 dhidi ya Etoile d'Or Mirontsy ya Comorro katika mchezo wa marudiano wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Kwa matokeo hayo sasa, Yanga imeweza kusonga mbele kwa jumla ya mabao 14-1 baada ya kuibuka na ushindi wa 8-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa wiki mbili zilizopita jijini, Dar es Salaam.

Yanga sasa itavaana na Al-Ahly ya Misri katika raundi ya kwanza ya mashindano hayo itakayochezwa mwezi Machi.

Mchezo ulichezwa katika uwanja wa Said Mohamed Cheikh ulioko mjini hapa, ambapo hakuna mawasiliano ya aina yoyote ya simu na uko kilomita 40 kutoka mji mkuu wa Comoro, Moroni.

Hata hivyo, Etoile ililazimika kutumia uwanja huo wenye nyasi bandia kutokana na kutokea katika kisiwa cha Anjoun, ambako hakuna uwanja wenye hadhi ya kimataifa.

Ngassa alikuwa "mwiba" wa Wacomoro, ambapo mara nyingi alikuwa akiwachachafya kwa chenga na mbio zake.

Aliweza kufunga mabao yake yote katika kipindi cha kwanza na baadae kutolewa na Kocha Dusan Kondic wakati kipindi cha pili kilipoanza.

Ngassa alizamisha bao lake katika dakika ya tatu wakati alipoweza kuunganisha mpira wa kona uliochongwa na Amir Maftah na kuongeza bao la pili mnano dakika ya 33 baada ya kuunganisha krosi ya Fred Mbuna.

Bao la mechi lilikuwa lile la tatu katika dakika ya 39, wakati alipoweza kuwalamba chenga mabeki wa Etoile kuanzia katikati ya uwanja na kuweza kuzamisha mpira wavuni.

Goli hili linaweza kufananishwa na lile la nyota wa zamani wa Argentina, Diego Maradona alilofunga dhidi ya England wakati wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 1986 nchini Mexico wakati alipowapiga chenga mabeki wanne wa England na kujaza mpira wavuni na timu yake kupata ushindi wa 2-1.

Ngassa alifunga mahesabu yake katika dakika ya 41 wakati alipounganisha krosi ya mshambuliaji Mkenya Boniface Ambani.

Vincent Barnabas aliifungia Yanga bao la tano katika dakika ya 77 wakati Ambani alimalizia bao la sita katika dakika ya 88 baada ya kuwahi mpira wa uliotemwa na kipa.




Source: Nipashe

No comments:

Post a Comment