Tuesday, February 3, 2009

JKT Ruvu yaishika koo Simba, yaambulia sare

PAMOJA na kuendeleza imani za ushirikina na kuzuia magari ya mashabiki yasiingie uwanjani kabla ya basi la wachezaji wao, haikutosha kuifanya Simba kupata pointi zote tatu baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 na JKT Ruvu katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Vituko vilitawala kwenye lango kuu huku viongozi wa Simba wakizuia magari yote kuingia kwenye geti hilo kwa madai kuwa walikuwa wanafanya mambo yao na kusababisha usumbufu kwa mashabiki waliofika uwanjani hapo na magari.

Baada ya tukio hilo timu ya JKT Ruvu walitumia geti dogo kuingia uwanjani wakitokea eneo la jukwaa lenye rangi nyekundu na baadaye wakiingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.

Simba iliyoanza kipindi cha kwanza kwa kasi na kufanya mashambulizi mengi golini kwa JKT, lakini washambuliaji wake Ulimboka Mwakingwe, Haruna Moshi pamoja na Musa Hassan Mgosi walipoteza nafasi katika dakika ya 34, 38 na 40.

Maafande wa JKT Ruvu walijibu mapigo katika dakika ya 41 na kupata bao la kuongoza kupitia Haruna Adolf aliyetumia vizuri uzembe wa mabeki wa Simba na kupiga shuti lililomshinda kipa Amani Simba na kufanya matokeo kuwa 1-0 hadi mapumziko.

Kipindi cha pili Simba walionekana kuwa makini zaidi na kufanya mashambulizi mengi zaidi golini kwa JKT katika dakika ya 47, Ulimboka Mwakingwe alishindwa kumalizia pasi nzuri aliyotegenezewa na Haruna Moshi 'Boban'.

Vijana hao wa Mtaa wa Msimbazi waliendeza kasi hiyo na kufanikiwa kupata penalti baada ya beki Buji Seleman kunawa mpira kwenye eneo la hatari.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Musa Hassani Mgosi alitumia vyema nafasi hiyo kwa kufunga bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 65 ya mchezo.

Mwisho wa mchezo huo kocha Partick Phiri aliwalaumu washambuliaji wake kwa kusoka umakini kwenye umaliziaji na kuahidi kulifanyia kazi tatizo hilo.

Naye kocha Charles Kilinda wa JKT Ruvu amemlalamikia mwamuzi wa mchezo huo Othman Kazi kwa kutokuwa makini na kuonyesha upendeleo zaidi kwa Simba.

Kwa matokeo hayo Simba imebaki kwenye nafasi ya pili na pointi zake 24 huku Yanga akiwa kileleni na pointi zake 39 wakati ligi inapoingia kwenye mapumziko leo hadi Marchi 14 kupisha maandalizi ya Taifa Stars kwa ajili ya fainali za mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) yatakayoanza kutimua vumbi baadaye mwezi huu.


No comments:

Post a Comment