Tuesday, February 3, 2009

Maximo atangaza kikosi cha Stars chenye wachezaji 27

Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ‘Taifa Stars’ Marcio Maximo amewaita wachezaji Mwinyi Kazimoto na Zahoro Pazi kwenye kikosi chake kwa ajili ya kujiandaa na fainali za michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) zitakazofanyika Ivory Coast kuanzia Februari 22 mwaka huu.

Kocha Maximo alitangaza kikosi chake Dar es Salaam jana, kikiwa na wachezaji 27 na kinatarajiwa kuingia kambini jijini hapa kesho kuanza maandalizi ya fainali hizo.

Zahoro Pazi anayechezea Mtibwa Sugar ambaye ni mtoto wa kipa wa zamani wa Simba ya Dar es Salaam, Idd Pazi ‘Father’, ndiye aliifunga Yanga bao pekee lililopatikana katika mchezo wa Kombe la Tusker hatua ya makundi Desemba mwaka jana, ambalo lilifanya matokeo ya kundi hilo la Yanga lililokuwa pia na timu ya URA ya Uganda yapatikane kwa njia ya kura, baada ya timu zote kuwa na pointi sawa.

Yanga ilitolewa katika utaratibu huo, hivyo Mtibwa na URA kutinga nusu fainali. Kazimoto ni kiungo mahiri wa JKT Ruvu, ambaye alijizolea sifa katika michuano ya Kombe la Taifa Mei mwaka jana iliyofanyika Dar es Salaam, akichezea timu ya Mkoa wa Pwani.

Hivi sasa Kazimoto anachezea JKT Ruvu na ni miongoni mwa wachezaji wanaong’ara katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Maximo alisema katika kikosi hicho cha wachezaji 27, amewarudisha baadhi ya wachezaji waliokuwa kwenye kikosi hicho na kuchezea michuano mbalimbali, lakini hawakuwemo katika timu iliyokuwa ikiwania kufuzu fainali za CHAN.

Aliwataja wachezaji hao kuwa ni Erasto Nyoni na Salvatory Ntebe ambao sasa wanachezea Azam ya Dar es Salaam, wakiwa wameongezwa katika usajili wa dirisha dogo, ambapo wakati wa michuano ya CHAN mwaka jana walikuwa wakichezea Vital’O ya Burundi.

Wachezaji wengine ambao hawakuwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kilichoshiriki michuano ya Chalenji, lakini wapo katika kikosi cha Taifa Stars ni beki Amir Maftah (Yanga), kiungo Jabir Aziz (Simba) na Uhuru Selemani (Mtibwa Sugar).
Pia katika kikosi chake, Maximo amemtema beki Meshack Abel wa Simba, ambaye alishiriki katika kuiwezesha Stars kufuzu fainali hizo. Wachezaji walioitwa tena katika kikosi hicho ni makipa Deogratius Boniventure ‘Dida’ kutoka Simba, Shaban Dihile (JKT Ruvu) na Farouk Ramadhan (Miembeni).

Walinzi ni Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga), Salum Sued (Mtibwa), Kelvin Yondani na Juma Jabu (Simba) Viungo ni Nurdin Bakari, Geofrey Bonny, Athumani Iddi, Abdi Kassim ‘Babi' (Yanga), Henry Joseph, Haruna Moshi (Simba) na Shaban Nditi wa Mtibwa.
Wakati washambuliaji ni Mussa Hassan ‘Mgosi’ (Simba), Jerry Tegete, Mrisho Ngassa, na Kigi Makasi kutoka Yanga, ambapo alisema atateua wachezaji 23 wa kwenda nao Ivory Coast.

Akizungumzia suala la kuitwa nahodha wa kikosi hicho, Henry Joseph ambaye yuko nchini Norway akifanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa, Maximo alisema mchezaji huyo akifuzu ataondolewa kikosini, lakini akikwama atakuwemo.

“Ukifanya uteuzi wa wachezaji chipukizi inakulazimu uwe na umakini wa hali ya juu, kwani chipukizi hao huwa na vipaji bila uzoefu, hivyo itawachukua muda kupata uzoefu kama wenzao,” alisema Maximo.

Pia alizungumzia suala la utaratibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuwapima wachezaji kubaini endapo wanatumia dawa za kuongeza nguvu, ikiwemo bangi na kusema kuwa suala hilo ni utaratibu wa kawaida na anaufurahia, kwani unafanya wachezaji wawe kama wa kulipwa na kuishi maisha ya kimichezo.

Pia kocha huyo alisema michuano hiyo ya CHAN itakuwa migumu kwa Stars, ambayo haipewi nafasi kubwa ya kufanya vyema, lakini aliwataka wadau wa soka kutambua kuwa kutopewa nafasi huko sio sababu ya kutofanya vizuri.

“Ni kweli hatupewi nafasi ya kufanya vyema kwenye CHAN ukilinganisha na timu kama Ghana na Senegal ambazo zina wachezaji wazoefu wa ndani ambao baadhi yao hata wamecheza kombe la dunia, lakini pamoja na hayo sisi sio vibonde,” alisema kwa msisitizo Maximo.

Stars itacheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe Februari 11, Dar es Salaam, ikiwa ni maandalizi ya fainali hizo. Katika kikosi cha jana, Maximo ameendelea kumuweka kando kipa mahiri nchini Juma Kaseja, ambaye wadau wengi wa soka wamekuwa wakipiga kelele awepo katika kikosi hicho.

“Sina tatizo na timu, naamini ipo siku nitacheza, bado umri wangu unaruhusu, najiamini nina uwezo wa kucheza, ipo siku nitawatumikia Watanzania,” alisema Kaseja jana kwa njia ya simu alipozungumza na HabariLeo. Kauli hiyo pia iliungwa mkono na Kocha Mkuu wa Villa Squad, Kenny Mwaisabula, aliyesema hajui kosa ambalo kipa huyo amelifanya kiasi cha kutoitwa katika kikosi hicho.

“Huyu bwana mdogo hakuua, sasa kosa gani ambalo halistahili kusamehewa? “Nadhani kulikuwa na haja ya kumsaidia mwalimu maana ni kwa manufaa ya Watanzania wote,“ alisema Mwaisabula.


No comments:

Post a Comment