Thursday, February 26, 2009

Wanajeshi wa Rwanda waondoka DRC


Maelfu ya wanajeshi wa Rwanda wameanza kuondoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kurudi nyumbani, wiki tano baada ya kuingia nchini humo kupambana na waasi wa Ki-hutu.

Kumekuwa na sherehe ya kuwapa mkono wa kwaheri huko Gomba, ambao ndio mji mkubwa zaidi mashariki mwa nchi.

Waziri wa mashauri ya nje wa Rwanda, alielezea kwamba oparesheni hiyo ya pamoja iliweza "kuwafanya hafifu kabisa" waasi wa FDLR.

Lakini msemaji wa BBC alisema vifo vingi vilitokea kwa upande wa raia.

Kuwepo kwa waasi hao katika jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ni kutokana na miaka mingi ya mzozo katika eneo hilo la Afrika.

Baadhi ya viongozi wa FDLR wanalaumiwa kuhusika katika mauaji ya watu wengi mwaka 1994, kabla ya kukimbilia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Rwanda mara mbili imeshawahi kuishambulia nchi hiyo jirani, ikielezea kwamba inawajibika kuwachukulia hatua wapiganaji hao, ambao wengi ni kutoka kabila la Hutu.

Mwezi Januari, nchi hizo mbili zilikubaliana kuchukua hatua za pamoja dhidi ya FDLR.

Wanajeshi wa Rwanda pia walimkamata kiongozi wa waasi, Laurent Nkunda, ambaye ni Mtutsi, ambaye anafikiriwa na viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuwa ni adui mkubwa.

Malori ya kijeshi pamoja, na vile vile wanajeshi 1,500 waliokuwa wakitembea kwa miguu waliweza kuvuka mpaka kufikia saa tisa za Afrika Mashariki.

Zaidi ya wanajeshi 3,000 wa Rwanda waliingia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mwezi Januari.

Viongozi wa Rwanda wanasema wanajeshi wote watakuwa wameondoka kufikia mwisho wa wiki hii.



Source: BBC

No comments:

Post a Comment