Bao la Jerry Tegete, dakika ya 57 limetosha kuiwezesha Yanga kuvunja ukuta mgumu wa Moro United na kuiacha timu hiyo ikihitaji mechi mbili za dakika 180 ili kujitangazia ubingwa.
Mpira wa Mrisho Ngassa kuelekea lango la wapinzani wao ulisababisha piga nikupige langoni mwa Moro United na kumpa nafasi Tegete kuandika bao pekee na muhimu,huku akimwacha kipa Haji Macharazi akichupa bila mafanikio.
Awali, United ilipania vilivyo kuchelewesha azma ya Yanga kujitangaza bingwa mapema baada ya kuigomea kwa dakika 45 za mchezo huo mkali uliofanyika jana katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ikicheza chini ya ukocha wa mchezaji na beki wa zamani wa Yanga, Fred Felix Minziro, Moro United ambayo ipo katika hatari ya kushuka daraja ilimudu kwa muda huo kuyazuia mashambulizi ya wachezaji wa Yanga na hivyo kwenda mapumziko zikiwa hazijafungana.
Mchezo huo mkali ulishuhudia timu hizo zikishambuliana na kusaka mabao na pointi, lakini safu za ulinzi za timu hizo zilikaa imara na kujaribu kuondosha hatari zote. Ukuta wa Moro United uliokuwa chini ya beki wa zamani wa Simba, Said Kokoo ulisimama imara na kuwazuia kwa muda washambuliaji wa Yanga.
Katika kipindi hicho, kila timu ilijitahidi kusaka bao, lakini bila mafanikio, ingawa kwa kiasi kikubwa Yanga ilionyesha zaidi dhamira ya kupata ushindi na kuhitaji ushindi katika mechi mbili ili kujitangaza bingwa.
Kwa upande wao, vijana wa Moro United walioko nafasi ya tisa ya msimamo wa ligi hiyo yenye timu 12 walikuwa imara na kuzima kiu ya washambuliaji wa Yanga.
Mchezaji wa zamani wa Yanga, Kudra Omari alikaribia kuipa bao timu yake dakika ya tatu ya mchezo huo kwa shuti kali ambalo hata hivyo lilipaa na kutoka nje.
Naye Tegete wa Yanga, dakika ya 11 alizubaa na kushindwa kupachika wavuni mpira baada ya pasi maridhawa ya Mrisho Ngassa huku Boniface Ambani akichezea nafasi, dakika 25 na 30 kwa mashuti ambayo yalitoka nje.
Kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Nizar Khalfan aliikosesha bao timu yake, dakika ya 43 kwa shuti kali ambalo lilipanguliwa na kipa Mzungu Obren Curkovic.
Kipindi cha pili, kocha Dusan Kondic aliwapumzisha Vincent Barnabas na Tegete na kuwaingiza Mike Baraza na Shamte Ally na Moro United ikimpumzisha Thomas Maurice na kuingia Samwel Ngassa, mabadiliko ambayo hayakubadili sura ya mchezo.
Baraza aliingia katika orodha ya waliokosa mabao baada ya dakika 76 za mchezo huo baada ya kubakia na kipa Macharazi na kukosa mbinu za kufunga bao kutokana na krosi ya Ngassa, lakini mpira huo ukampita.
Kosa kosa ziliendelea kwa pande zote mbili, huku Kudra akitikisa nyavu dakika ya 80, lakini mwamuzi Owden Mmbaga alilikataa bao hilo kwa madai ya kuotea.
Minziro alieleza baada ya mchezo kuwa timu yake ilistahili sare ya bao 1-1, lakini uamuzi mbovu umeiathiri. Kocha huyo alionyesha hasira na kukaribia kumwaga chozi baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo huo.
"Bao la Kudra lilikuwa safi, inashangaza kuona mwamuzi amelikataa. Waamuzi wapunguze ushabiki wao, vinginevyo wanaimaliza soka ya Tanzania," alidai.
Dusan Kondic wa Yanga alieleza kuwa hawezi kuuzungumzia mchezo wowote hadi abakiwe na mchezo mmoja kabla ya kutangaza ubingwa.
Ligi hiyo imeahirishwa kwa muda hadi Machi ili kuipa nafasi timu ya taifa, Stars kujiandaa na michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) zitakazofanyika nchini Ivory Coast baadaye mwezi huu.
No comments:
Post a Comment