Taarifa kutoka Madagascar, zinasema takriban watu watano wameuawa baada ya askari polisi kuwafyatulia risasi waandamanaji wa upinzani katika mji mkuu Antananarivo.
Hata hivyo taarifa nyingine zinasema watu waliouawa wanafikia ishirini na watano.
Kumekuwa na upinzani mkali nchini humo dhidi ya hatua ya kufukuzwa Meya wa mji wa Antananarivo Andry Rajoelina, ambaye amekuwa katika harakati za kuwania madaraka na rais wa nchi hiyo.
Meya aliyetimuliwa amekuwa akimtuhumu rais Marc Ravalomanana kwa kufuja fedha za umma na kuendeleza udikteta.
Kwa mujibu wa afisa mmoja mwandamizi wa jeshi la polisi aliyenukuliwa na shirika la habari la Reuters, inawezekana watu 25 wameuawa.
Waandamanaji walikuwa wanaelekea katika makazi ya Rais Ravalomanana ndipo polisi wa kuzuia ghasia walipofyatua risasi.
Mapema wakati wa maandamano hayo yaliyohudhuriwa na watu 20,000, wafuasi wa Meya wa zamani walimtangaza kuwa ni kiongozi wa serikali ya mpito ya nchi hiyo.
Bwana Rajoelina alifutwa kazi na serikali siku ya Jumanne na nafasi yake imechukuliwa na Guy Randrianarisoa.
Bwana Rajoelina, ambaye amefanikiwa kuisumbua serikali kutokana na utendaji mbovu, amesema ataunda serikali ya mpito kama rais President Marc Ravalomanana hatojiuzulu.
Madagascar, ambacho ni kisiwa kikubwa cha nne duniani, kwa muda mrefu kimekuwa kikitembelewa na watalii na kituo cha makampuni mengi ya kigeni, hivi sasa kimo katika harakati za kutafuta mafuta, madini ya shaba na uranium.
Source: BBC
No comments:
Post a Comment