Wednesday, March 25, 2009

Zanzibar bingwa tena judo

Zanzibar juzi ilitetea ubingwa wake wa mchezo wa judo kwa nchi za Afrika Mashariki baada ya kuibuka washindi wa jumla katika michuano iliyoshirikisha mataifa manne. Zanzibar ilitwaa ubingwa huo kwa mara nyingine, baada ya kushinda medali sita za dhahabu na fedha pamoja na shaba nne, wakati Kenya ilishika nafasi ya pili kwa kupata medali moja ya dhahabu, fedha nne na shaba tano.

Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Burundi ambayo ilishinda medali moja ya dhahabu fedha tatu na shaba nne na Tanzania Bara ilishika mkia ikiwa imepata medali moja ya fedha na shaba mbili. Pamoja na kuibuka mabingwa Zanzibar pia ilitoa mchezaji bora wa michuano hiyo ambaye alikuwa ni Masoud Amour Kombo, wakati katika mashindano yasiyo rasmi ya wanawake mchezaji, Munezero Antoinette kutoka Burundi alichaguliwa kuwa mchezaji bora.

Zaidi ya mataifa kumi yalikuwa yamealikwa kushiriki michuano hiyo ya tatu, lakini ni mataifa manne tu ndio yalishiriki kwenye michuano hiyo ambayo ni Burundi, Kenya, Tanzania Bara na wenyeji Zanzibar. Balozi wa Japan nchini Tanzania, Hiroshi Nagawa alikuwa mmoja wa wageni waliohudhuria michuano hiyo.



Source: HabariLeo

No comments:

Post a Comment