Monday, March 16, 2009

Yanga Yalala Kwa Al Ahly

Mshambuliaji flavio Amando (kushoto) wa Al Ahly ya Misri akiwa chini ya ulinzi wa kiungo Godfrey Bonny wa Yanga ya Tanzania, wakati wa mechi ya ligi ya mabingwa iliyocheza mjini Cairo.

MABINGWA watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly wameanza kampeni ya kutetea taji la kwa kishindo kwa kuisambarati Yanga kwa mabao 3-0 katika mchezo uliochezwa jijini Cairo, Misri.

Mshambuliaji Mohamed Barakat alikuwa mwiba mkali kwa ngome ya Yanga kwa kuifungia Al Ahly mabao mawili pamoja na lile la mapema zaidi katika sekunde ya 44 mwanzoni mwa mchezo.

Mabingwa hao watetezi aliouanza mchezo kwa kasi na kutawala vyema sehemu ya kiungo walipata bao hilo la mapema kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Misri, Mohamed Barakat akipokea pasi ya Muhtaz Ino na kupachika mpira wavuni.

Kuingia kwa bao hilo kuliamsha ari ya Yanga ilijibu shambulizi katika dakika ya pili kupitia mshambuliaji wake Bonifase Ambani aliyekosa bao la wazi kwa kushindwa kuunganisha pasi nzuri ya Mrisho Ngasa.

Baada ya kosa kosa hiyo mabingwa hao wa Afrika, Al Ahly waliutawala mchezo kwa zaidi ya dakika 16 Yanga ilifanikiwa kufika langoni kwa Wamisri hao mara moja, huku mashambulizi yao yote yakipitia upande wa kulia na kumpa wakati ngumu beki Amri Maftah.

Kipa Obren Cirkovick ilimbidi kufanya kazi ya ziada kuokoa mpira wa kichwa uliopigwa na Ahmad Bilal katika dakika ya 12.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Angola, Flavio alitumia vizuri uzembe wa kipa Obren aliyeshindwa kuokoa kwa umakini krosi ya Barakat na kumkuta mfungaji dakika ya 20 kufanya matokeo kuwa 2-0 hadi mapumziko.

Al Ahly wakionekana wameisoma vizuri Yanga na kutumia udhaifu wa beki za pembeni walipata bao la tatu lilofungwa tena na Mohamed Barakat aliyeunganisha vizuri krosi ya Ahmad Faraj katika dakika ya 53.

Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya kocha Dustan Kondic alifanya mabadiliko kwa kumtoa Godfrey Bonny, Ben Mwalala na Mrisho Ngassa na nafasi zao kuchukuliwa na Geogre Owino, Jerryson Tegete na Mike Baraza.

Mabadiliko hayo yalirudisha uhai wa Yanga na kufanya mashambulizi mengi na kushuhudia mashuti ya Bonifase Ambani na Nurdin Bakari yakigonga mwamba katika dakika 79 na 80, huku Mike Baraza akikosa bao yeye na kipa kwa shuti lake kupaa juu.

Kwa matokeo haya Yanga sasa inahitaji kushinda mabao 4-0 kama inataka kusonga mbele kwa raundi ya 16 bora msimu huu, matokeo mengine yoyote watabaki na kumaliza hadithi ya Tanzania katika michuano ya kimataifa kwa mwaka huu.



Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment