Monday, March 9, 2009

Congo wafalme wapya Afrika CHAN 2009

DR CONGO imeweka historia kwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani CHAN kwa kuifunga Ghana kwa mabao 2-0.

Ghana iliyoshuka dimbani na kumbukumbu nzuri ya kuifunga Congo 3-0 katika mchezo wa mwisho wa Kundi A na kupewa nafasi kubwa ya kuwa bingwa wa michuano hiyo, lakini mambo yaliwaendea kombo.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili Congo ilipata bao la kwanza kupitia kwa Deopa Kalimtupa aliyeunganisha vizuri mpira wa krosi kwa kichwa na kushinda kipa wa Ghana, Makafi.

Kuingia kwa bao hilo kuliamsha hali ya Ghana ambao wanasifa nzuri ya kusawazisha mabao kila wanapofungwa katika michuano hii, lakini mashambulizi yao yaliishia mikoni mwa ngome imara ya vijana wa Kabila.

Ghana wakiendeleza mashambulizi ya kutafuta bao la kusawazisha walijisahau na kufungwa bao la pili kwa krosi ya Mputu iliyomkuta John Bedi aliyepiga shuti lilomshinda kipa Makafi na kufuta ndoto ya Black Stars kutwaa ubingwa huo.

Juzi timu ya taifa ya Zambia, Chipolopolo ilithibitisha kwamba iliteleza tu kwa kushindwa kufika fainali baada ya kufanikiwa kuwafunga Senegal kwa mabao 2-1 na kutwaa nafasi ya tatu ya michuano hiyo.

Huku mshambuliaji wake Given Singuluma akiwa mfungaji bora wa michuano hiyo kwa kufunga mabao matano.


Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment