WAZIRI kiongozi wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Mohamed Gharib Bilal, ameamua kushika chaki na kufundisha wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Mwanasiasa huyo sasa anafundisha somo la fizikia na pia anawafundisha mbinu za kulifundisha somo hilo kwa walimu wanaoanza kazi ya kufundisha kwenye chuo hicho.
“Nafasi ninayo; chuo hiki ni cha Watanzania. Nimeona vema kuwapatia wengine ujuzi wangu ili waendeleze taifa,” alisema akiwa katika moja ya ofisi za chuo hicho juzi jioni alipozungumza na Mwananchi
Kitaaluma, kiongozi huyo wa zamani ni mwanasayansi aliyebobea, hususani katika masuala ya atomu (atomic).
Dk. Bilali, ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza la Udom, alisema anaona fahari kufundisha vijana kutokana na ukweli kwamba chuo hicho ni cha hadhi ya aina yake na ni kizuri. Chuo hicho kinajengwa na serikali kwa kutumia fedha za hapa nchini kikiwa na malengo ya kuwaendeleza Watanzania.
Alisema Udom ni chuo cha kipekee kwa nchi za Afrika Mashariki na kwamba anaona fahari kuwa karibu na chuo hicho kutokana na malengo mazuri ya serikali ya CCM.
“Udom ni moja ya kazi nzuri zinazofanywa na serikali," alisema. "Ni chuo cha kujivunia na kitakuwa na matunda mazuri sana kwa taifa.”
Aliwapongeza wafanyakazi wenzake, wakiwemo wahadhiri wanaoongozwa na makamu mkuu wa chuo, Profesa Idris Kikula kwa ushirikiano wanaouonyesha katika kukiendeleza chuo hicho na kuwataka waendelee kuimarisha mshikamano ili kufanikisha malengo yote.
Awali, Kikula aliiambia Mwananchi ofisini kwake kuwa Dk. Bilal ameonyesha mfano kwa viongozi nchini kulisaidia taifa kwa kuendeleza vijana.
Alisema Dk. Balal pamoja na wadhifa aliokuwa nao awali na sasa akiwa mwenyekiti wa baraza la chuo, anafanya kazi ya kufundisha ili kurithisha vijana ujuzi wake.
Udom pia ilimpokea waziri wa zamani wa Kenya, Profesa Amakuwa Anangwe ili afundishe chuoni hapo.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment