Sunday, March 22, 2009

Kiongozi mpya wa Madagascar Andry Rajoelina Kiongozi wa Madagascar aapishwa


Madagascar yaapisha kiongozi mpya

Andry Rajoelina, mtu aliyemuondoa madarakani Rais Marc Ravalomanana mapema wiki hii, ameapishwa rasmi kushika hatamu za uongozi za kisiwa hicho kikubwa barani Afrika kilicho Bahari ya Hindi.

Maelfu ya wafuasi wake walihudhuria sherehe za kumuapisha zilizofanyika katika uwanja wa michezo mjini, Antananarivo, lakini hata hivyo wanadiplomasia wengi walisusia.

Siku ya Ijumaa Marekani ilisimamisha misaada isiyo ya kibinadamu kwa Madagascar na halikadhalika Muungano wa Afrika-AU ukaisimaisha uanachama.

Wiki hii mahakama kuu kabisa ya Madagascar iliidhinisha mabadiliko ya uongozi ya nchi hiyo.

Msaidizi wa kiongozi aliyeondolewa madarakani Bwana Ravalomanana, amesema aliambiwa na mabalozi wa Marekani, Ufaransa, Ujerumani na Muungano wa Afrika, wamemwambia hawatohudhuria sherehe hizo.

Takriban wafuasi 2,000 wa Bwana ravalomanana, imearifiwa wamefanya maandamano mjini Antananarivo katika uwanja wa Demokrasi kuipinga serikali mpya.

Mwandishi wa BBC Christina Corbett aliye mjini Antananarivo amesema upinzani dhidi ya utawala wa Bwana Rajoelina unaoungwa mkono na jeshi, haujamzuia kufanya sherehe ya kifahari ya kuapishwa.

Wasaidizi wa Bwana Rajoelina amesema hawasumbuliwi na juhudi za kimataifa za kuipinga serikali yao kufuatia kuondolewa madarakani Bwana Ravalomanana.

Bwana Rajoelina, mwenye umri wa miaka ambaye aliwahi kuwa disco joka, amesimamisha shughuli za bunge na ameunda serikali ya mpito kukiongoza kisiwa hicho kilicho Bahari ya Hindi.



Source: BBC

No comments:

Post a Comment