Tuesday, March 17, 2009

Wachezaji Yanga wadai kuhujumiwa

Nahodha wa Yanga Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari wakati waliporejea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam jana wakitokea Misri walikocheza na Al Ahly katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Baadhi ya wachezaji wa Yanga wamesema kwamba wanahisi kulikuwa na hujuma katika mechi yao ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri. Katika mechi hiyo iliyofanyika Jumapili iliyopita mjini Cairo Misri, wawakilishi hao wa Tanzania walifungwa mabao 3-0.

Wakizungumza jana asubuhi kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kuwasili kutoka Misri wachezaji hao ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini walisema kabla hawajaenda Misri maandalizi yalikuwa hafifu.


“Tunahisi kama ni hujuma ilianzia hapahapa maana kabla hatujaondoka, hata maandalizi hayakuwa makubwa yaani kama vile ilivyozoeleka watu mnapokutana na timu kubwa,”alisema mchezaji mmoja tegemeo wa timu hiyo.

“Maandalizi yalikuwa mabovu wachezaji mara tuhamishwe hotelini tulitoka Lamada tukapelekwa Mwenge tukawa tunalala wanne wanne, mara wengine wasipewe posho kulikuwa na mambo ambayo hatukuyaelewa kabisa,”alisema.

Aidha, mchezaji mwingine ambaye pia huchezea timu ya taifa alisema hata upangwaji wa timu hakuuelewa. “Sikuelewa kabisa upangwaji wa timu kitendo cha Kondic (Dusan Kocha wa Yanga) kushindwa kumpanga Jerry Tegete tangu mwanzo sikuelewa kabisa badala yake alimpanga katika kipindi cha pili na dakika zilibaki chache…


“Na alipoingia tuliona mabadiliko hivyo angeingia mapema ama angeanza pengine tusingefungwa mabao yote hayo, lakini sisi tunamwachia kocha yeye ndiyo mwamuzi wa kila kitu bwana,”alisema mchezaji huyo. Hata hivyo viongozi waliofuatana na timu hiyo hawakuwa tayari kulizungumzia hilo kwani Katibu Mkuu Lucas Kisasa alikataa kuzungumza na waandishi na kuondoka zake.

Badala yake Mwenyekiti wa Yanga Iman Madega aliizungumzia mechi ya marudiano itakayofanyika mwisho wa mwezi huu ambapo hata hivyo alipingana na kocha wake Kondic. Madega alisema kwa sasa wanaisubiri timu hiyo kwa mechi ya marudiano na kuahidi kufanya vyema na kwamba timu inaanza kujifua na kufungwa mechi ya kwanza hakujawakatisha tamaa.

Lakini Kondic alisema mechi hiyo itakuwa ngumu kwao kwa kuwa Al Ahly ni timu nzuri na inafanya vyema zaidi. Kondic ambaye ameonekana kukata tamaa alisema Al Ahly ni nzuri na itakuwa mechi ngumu kutokana na timu hiyo kuwa imesheheni wachezaji wataalamu zaidi.



Source: HabarLeo

No comments:

Post a Comment