Friday, March 13, 2009

Wafanyakazi wa misaada wakamatwa Darfur

Wakimbizi zaidi ya milioni mbili wanasaidiwa na mashirika ya misaada Darfur


Wafanyakazi watatu wa shirika la madaktari wasio na mipaka la Medecins sans Frontieres-MSF tawi la Ubelgiji, wametekwa nyara eneo la Darfur nchini Sudan.

Shirika hilo la MSF limesema wafanyakazi wake hao watatu walitekwa nyara pamoja na wafanyakazi wa shirika hilo wenye asili ya Sudan ambao baadae waliachiliwa huru siku ya Jumatano kaskazini mwa Darfur.

Utekwaji nyara huo umetokea baada ya serikali ya Sudan mapema mwezi huu kuamuru kutimuliwa vikundi 13 vya kutoa misaada pamoja na wafanyakazi wa MSF wa Ufaransa na Uholanzi.

Waliamriwa kuondoka baada ya Rais wa Sudan Omar al-Bashir kutakiwa kujibu mashtaka mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC).

Anatuhumiwa kuhusika na uhalifu wa kivita na uhalifu mwengine dhidi ya ubinadamu katika jimbo la Darfur.

Wafanyakazi hao wa kutoa misaada walitekwa siku ya Jumatano jioni wakiwa wameelekezewa mtutu wa bunduki kutoka ofisi zao zilizopo Saraf Umra, umbali wa kilometa 230 katika mji mkuu wa jimbo la magharibi mwa Darfur wa El Fasher.

MSF limesema mateka hao akiwemo muuguzi kutoka Canada, daktari kutoka Italia na mratibu Mfaransa.

Wafanyakazi wawili wa rais wa Sudan nao walitekwa lakini wakaachiliwa huru baadae.

MSF imeeleza haina taarifa zaidi na haitazungumza zaidi kwa ajili ya kulinda usalama wa wafanyakazi wake.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC wa Afrika Mashariki Karen Allen eneo wanalofanyia kazi mashirika ya kutoa msaada, ni la hatari kwa kukabiliwa na vitendo vya ujambazi.



Source: BBC

No comments:

Post a Comment