Thursday, March 19, 2009

Mn'goe Rais wa Somalia - Bin Laden

Osama Bin Laden


Osama Bin Laden katika sauti iliyo rekodiwa na kutumwa kwenye mtandao wa internet, ametoa wito wa kun'golewa kwa rais mwenye msimamo wa kati wa Somalia.

Bin Laden amesema Rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed "amebadilika na kuungana na kafiri".

Bw Ahmed aliapishwa mwezi Januari baada ya mazungumzo ya upatanishi yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa, na kuahidi kuanzisha matumizi ya sheria ya dini ya Kiisilam, katika nchi hiyo yenye Waisilam wengi.

kupingana

Hata hivyo kundi la al-Shabab ambalo lina uhusiano na al-Qaeda limeendelea kupigana na rais huyo.

Waandishi wa habari wanasema sauti hiyo, haikuweza kuthibitishwa mara moja ni ya nani, lakini inafanana na ya Bin Laden na imerushwa kupitia mitandao inayofahamika ya wapiganaji.

Wito huo uliorekodiwa kwa dakika 12, na kupewa kichwa cha habari kisemacho "Endeleeni kupigana, mabingwa na Somalia" umeambatana na picha ya Bin Laden na ramani ya Somalia ikionekana nyuma ya picha hiyo.

maadui zetu

Uchaguzi wa kiongozi huyo wa Somalia "ulichochewa na mjumbe wa Marekani nchini Kenya" umesema ujumbe huo.

Aidha, ujumbe huo umeendelea kumtuhumu Bw Ahmed kwa "kubadilika na kuwageuka ili kuungana na kafiri" katika serikali ya umoja wa kitaifa.

"Huyu Sheikh Sharif lazima aondolewe" umesema ujumbe huo, kabla ya kumfananisha kiongozi huyo wa Somalia na "marais wa Kiarabu wanaolipwa na maadui zetu".

Bw Ahmed alikuwa kiongozi wa kundi lijulikanalo kama Mahakama za Kiisilam ambalo lilikuwa likidhibiti mji wa Mogadishu mwaka 2006 kabla ya kutimuliwa na majeshi ya Ethiopia yaliyokuwa yakimuunga mkono rais aliyepita wa Somalia.



Source: BBC

No comments:

Post a Comment