Thursday, March 12, 2009

Taasisi, wadau watofautiana kupigwa kwa Mwinyi

TUKIO la kijana Ibrahim Said kumpiga kofi Rais mstaafu wa awamu ya pili al-haji Ali Hassan Mwinyi, limepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya taasisi hapa nchini.

Taasisi hizo ni pamoja na Baraza la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Hali kadhalika baadhi ya watu binafsi waliozungumza na Mwananchi, wamepokea habari za tukio hilo, kwa mitazamo tofauti Kwa upande wake Baraza la Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, limesema mzee Mwinyi alitengeneza mseto usiolika kwa waislaamu.

Hata hivyo chombo hicho, kimewataka Watanzania kuzingatia ujumbe uliomo ndani ya kibao alichopigwa mzee Mwinyi na si kujadili kupigwa kwake.

Katibu mkuu wa baraza hilo, sheikh Ramadhan Sanze alisema, mzee Mwinyi aliwatengenezea Waislaam mseto usiolika kwa kutumia mafundisho ya dini na siasa kwa namna isiyofaa kidini, katika vita dhidi ya Ukimwi.

"Mzee Mwinyi alishindwa kuyafahamu mazingira yaliyokuwa yamemzunguka na ufahamu wa waumini waliokuwepo.

Hivyo akawatengenezea mseto usiolika na kujaribu kuwashawishi waislaam waukubali," alisema sheikh Sanze na kuongeza: "Katika Uislaam zinaa haina dharura na tumeambiwa tusiikaribie kabisa na sio tusizini.

Lakini kwa uelewa wetu Mwinyi alijaribu kuonesha kuwa zinaa ina dharura na kwamba mtu akibanwa sana anaweza kuzini lakini kwa kutumia kondomu jambo ambalo ni kinyume kabisa na uislaam".

"Kwa maana hiyo ukishaonesha kuwa zinaa ina dharura, basi utakuwa umepingana na uislaam yaani Qur-an na sunna (mwenendo na tabia) za Mtume Muhammad (SAW) ambaye tunasherehekea kuzaliwa kwake".

Hata hivyo Sanze alisema, kondom sio kinga ya Ukimwi huku akirudi katika historia kwa kusema kuwa Ukimwi uligundulika nchini mwaka 1983 kwa kuwa na wagonjwa watatu.

Alifafanua kuwa, watanzania waliijua kondom baada ya kugundulika kwa maradhi hayo lakini cha kushangaza kadiri siku zinavyokwenda maambukizi yanazidi kuongezeka licha ya kuongezeka kwa matumizi ya kondom.

"Kwa hiyo kidini mzee Mwinyi alifanya kosa na hata kitaalamu pia amefanya kosa kwa sababu takwimu zinapingana naye kwamba kondom ni kinga ya Ukimwi," alisema.

Alisema shughuli aliyokuwa akihutubia Mwinyi ni ya waislaam na wala haukuwa mjadala, jambo ambalo kwa tafsiri ya haraka haraka kauli yake ni kama fatwa (hukumu) jambo ambalo lingetafsiriwa vibaya na wasiokuwa waislaam.

Hata hivyo Sanze aliwataka wanasiasa nchini wasome alama za nyakati na kuchagua cha kuwambia waislaam wanapowalika katika shughuli zao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislaam, sheikh Ponda Issa Ponda alisema, kauli ya mzee Mwinyi inaonyesha kiwango cha juu kabisa cha mmomonyoko wa maadili nchini.

Lakini aliwataka Watanzania kuzingatia ujumbe uliomo ndani ya kofi alilopigwa kiongozi huyo mstaafu na si kujadili kupigwa kwake.

"Cha kuzingatia hapa ni ujumbe uliomo ndani ya kile kibao alichopigwa na si kujadili kupigwa kwake" alisema sheikh Ponda.

Alisema mashirika yanayofanya biashara ya mipira hiyo ya kufanyia zinaa yameanza kuwatumia watu maarufu ikiwa ni pamoja na marais wastaafu ili kuwatangazia biashara zao.

"Mzee Mwinyi ameingia katika mkumbo huo wa kutangaza biashara za mashirika hayo.

Kimsingi anajua kuwa zinaa ni haramu katika uislaam na yeye mwenyewe alithibitisha hayo alipokuwa akihutubia.

Lakini aliamua kuifanyia ‘publicity’ kondom kwa maslahi yake na maslahi ya hao anaowatangazia biashara zao|" alisema na kuongeza:

Lakini baraza hilo likiunga mkono hatua ya Ibrahimu, Bakwata kwa upande wake imesema tukio hilo ni kifedheha na linapaswa kulaaniwa vikali.


Katika taarifa yake, Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Issa bin Shaaban Simba alisema kitendo ni cha aibu na uhuni mkubwa.

"Tunapenda (Bakwata) kutoa tamko la kulaani kitendo hiki cha aibu, fedheha na cha kihuni kilicho fanywa na kijana mmoja wakati wa Baraza la Maulid, jijini Dar es Salaam jana (juzi),"alisema Sheikh Simba Alisema Bakwata, imesikitishwa na hatua ya kijana huyo kufanya kitendo hicho kinachopingana na misingi ya ustaarabu.

"Tunaomba radhi kwa mheshimiwa Alhaji Mwinyi pamoja na familia yake na kwa kuwa swala lenyewe hivi sasa lipo mikononi mwa vyombo vya dola kwa uchunguzi, ni matarajio ya kila Mtanzania litaeleweka kwa undani na mtuhumiwa kufikishwa mbele ya haki,"alisema Sheikh Simba.

Kauli kama hiyo, imetolewa pia na Umoja wa Vijana wa UVCCM ambapo pamoja na kulaani tukio hilo, pia umevitaka vyombo vya ulinzi na usalama viimarishe ulinzi kwa viongozi wastaafu na waliopo madarakani, ili mambo kama hayo yasijitokeza tena.

Jumuiya hiyo imesema ulinzi usipoimarishwa, kuna uwezekano wa kutokea kwa tukio kama hilo katika shughuli nyingine zinazoshirikisha viongozi wa kitaifa.

Tamko hilo lilitolewa jana na Mwenyekiti wa UVCCM,Yusufu Hamad Masauni, kwa niaba ya Baraza Kuu la umoja huo linaloendelea na kikao chake mjini hapa.

Masauni alisema kitendo hicho ni cha kihuni, fedheha, utovu wa nidhamu na udhalilishaji wa maadili ya dini zote na utamaduni wa kitanzania.

“Kitendo hicho si tu kwamba kimemdhalilisha Mzee Mwinyi, lakini pia kimewasononesha vijana wa CCM kote nchini na watu wote wanaomfahamu.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi, walisema kitengo kilichofanywa na mtu huyo si cha kawaida hata kama aliudhiwa na kiongozi huyo.


Kutoka Tanga Burhani Yakub, anaripoti kuwa Mbunge wa zamani wa Mlalo wilayani Lushoto,Charles Kagonji, ameeleza kusikitishwa kwake na tukio hilo.

Akizungumza na Mwananchi Mbunge huyo alisema tukio hilo ni la kulifedhehesha taifa na akataka uchunguzi wa kina ufanyike ili kujua chanzo hicho.

Kagonji alisema tukio kama hilo ni la aibu kwa taifa hali na kwamba hali hiyo inaashiria kuwa ulinzi ni hafifu.

Jijini Dar es Salaam, wananchi waliwatupia lawama kitengo cha ulinzi wa kiongozi huyo kuwa kimeonyesha udhaifu mkubwa kiasi cha kuruhusu mtu kutoka kwenye umati wa watu na kupanda jukwaani kumpiga kiongozi.

Ashim Shabani wa Sinza alisema kitendo hicho ni cha fedheha kwa maafisa usalama na kuwataka wajipange upya katika shughuli zao.



Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment