Tuesday, March 31, 2009

Didier Drogba aleta maafa kwao Ivory Coast

Mmoja kati ya mamia ya vijana waliojeruhiwa katika pambano kati ya timu ya Ivory Coast na Malawi akiwa amebebwa kupelekwa eneo la matibabu katika mechi iliyofanyika Jumapili katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

UJIO wa nyota wa Ivory Coast, Didier Drogba katika kikosi cha taifa, The Elephants umeelezwa kuwa uliwachochea mashabiki kufurika uwanjani kuishangilia timu hiyo.

Mashabiki wapatao 50,000 wanasemekana katika Uwanja wa Felix Houphouet Boigny kuiona timu yao ikicheza na Malawi, lakini kabla ya kumalizika kwa mchezo huo, ukuta mmoja uliporomoka na kusababisha hofu, vurugu miongoni mwa mashabiki.

Uwanja huo una uwezo wa mashabiki 35,000. Taarifa zilizopatikana jana zilieleza kuwa mashabiki 22 walikufa na wengine 134 kujeruhiwa.

Drogba ambaye alikuwa nje ya kikosi hicho kwa muda mrefu alipachika mabao mawili, mengine yakifungwa na Salomon Kalou na Christopher Ndri Koffi anayecheza Olympique Marseille ya Ufaransa.

Rais wa Shirikisho la Soka la Ivory Coast (FFF), Jacques Anouma ametaka utulivu wakati uchunguzi ukiendelea kuhusiana na tukio hilo.

"Tunasikitishwa na kile kilichotokea, lakini kwa sasa hatuwezi kusema lolote, tusubiri uchunguzi," Anouma aliliambia gazeti la Le Patriote.

"Tusubiri matokeo ya uchunguzi huo kama ambavyo umeanzishwa na Waziri wa Usalama.

Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa, Sepp Blatter ameeleza kushtushwa na tukio hilo na kutaka FFF wachunguze na kuwasilisha kwao haraka ripoti ya uchunguzi huo.



Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment