Saturday, March 28, 2009

Papa Benedict ajipata matatani

Papa Benedict ajipata matatani kwa sababu ya Kondom

Papa Benedict wa kumi na sita amelaumiwa vikali kwenye tahariri iliyoandikwa kwenye jarida mashuhuri zaidi duniani la utabibu Lancet kuhusiana na matamshi yake kuhusu mipira ya kondom.

Jarida hilo linasema kuwa Papa alipotosha ushahidi wa kisayansi alipohoji uwezo wa mipira ya kondom kuzuia kusambaa kwa virusi vya HIV akisema kuwa mipira ya Kondom inachangia zaidi kuenea kwa virusi hivyo.

Sasa inaonekana jaribio la Papa Benedict kuhalalisha mafunzo ya kanisa Katoliki kuhusu matumizi ya mipira ya Kondom limeambulia patupu.

Papa aliyatoa matamshi haya wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye ndege yake akiwa njiani kwa ziara barani Afrika ambapo maradhi ya ukimwi yameua na yanaendelea kuua mamilioni ya watu, alinukuliwa kusema kwamba maradhi hayo ni changamoto isiyodhibitiwa kwa kusambaza mipira ya kondom.

Aliongeza kwamba mipira ya kondom inasaidia kusambaza zaidi virusi vya HIV.tahariri ya jarida la Lancet ilielelezea matamshi ya Papa kuwa ya kutisha na yasio ya uhakika na kwamba Papa alipotosha ushahidi wa kisayansi ili kupigia debe imani za kanisa Katoliki.

Matamshi haya yanaonekana kumponza kwani sasa jarida la Lancet katika tahariri yake linasema kwamba sio bayana iwapo kosa la Papa lilitokana na kutojua au jaribio maksudi la kutumia sayansi ili kupata uungwaji mkono wa imani ya Kanisa Katoliki.

Linasema kwamba kwa maoni bora zaidi ya utatibu ni kuwa mipira ya condom inayotumiwa na wanaume ndio njia ya pekee mfuti kabisa kuzuia maambukizi ya virusi vya HIV.

Hadi sasa, washauri wa Papa Benedict kuhusu masuala ya uhusiano wa umma wa Papa Benedict wameshindwa kupata ushahidi wowote ulio kinyume na hayo.



Source: BBC

No comments:

Post a Comment