Sunday, March 22, 2009

Mama wa aliyempiga Mwinyi amwomba Kikwete amsaidie

*Adai ana hali mbaya gerezani

MAMA mzazi wa kijana Ibrahim Said aliyempiga kibao Rais mstaafu Mwinyi, jana alitinga Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) kumsihi Mufti wa Tanzania, Sheikh Issa Bin Shaaban Simba, akamuombe Mzee Mwinyi na Rais Jakaya Kikwete kumnusuru kijana wake kwa vile afya yake hairidhishi gerezani.

Mama huyo mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam alifika katika ofisi za Bakwata, Kinondoni baada ya kutoka Gereza la Keko kumuona mtoto wake.

Akizungumza na waandishi huku akibubujikwa na machozi, Rehema alisema hali aliyomkuta nayo mwanaye ni mbaya na hairidhishi.

Ibrahim Said (26) alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kutokana na kosa la kumshambulia kwa kumnasa kibao Mzee Mwinyi, alipokuwa akihutubia Baraza la Maulid lililofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam Machi 9 mwaka huu.

Rehema alidai kijana huyo anaumwa na amevimba mwili kutokana na kipigo na adhabu nyingine anazopata katika gereza hilo. "Nimekuja kumuomba Mufti akamuombe rais, mwanangu apunguziwe adhabu au ikiwezekana amsamehe na kutoka gerezani, kwa kuwa yeye ni mkuu wa nchi na anayo mamlaka hayo,” alisema na kuongeza: "Kosa alilofanya mwanangu ni kama ajali tu, na yeyote inaweza kumpata.

Lakini naumia sana kutokana na hali aliyonayo gerezani hata kutembea hawezi anaburuzwa na kipigo kimeongezeka”. Alilalamika kuwa mwanaye hatendewi haki kwa kuwa anaumwa huku mwili wake ukiwa umevimba kwa kipigo bila hata kupatiwa huduma ya dawa na chakula.

"Hatendewi haki, hapewi kula, anaumwa hapewi dawa, anapigwa na kuteswa mwanangu,” alilalamika.

Aidha mama huyo aliwataka watu wasiende kumtembelea kijana wake katika Gereza la Keko kwa kuwa wanazidi kumchanganya.

"Nawaomba watu wasimtembelee, kwa kuwa kila anapotembelewa namna hiyo, anazidi kuchanganyikiwa,” alisema Rehema na kumshukuru Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salim kwa kumsaidia kwenda kumuona Mufti Simba.

Baada ya kufika kwa Mufti na kueleza matatizo yake, Sheikh Simba alimuamuru Afisa Habari wa Bakwata Issa Mkalinga kuita waandishi ili mama huyo aongee nao na kutoa malalamiko yake.

Kwa upande wake, Mufti Simba aliahidi kuyafikisha maombi ya mama huyo kwa Rais Kikwete na Mzee Mwinyi.

"Mimi niliomba radhi siku ile ile kwa Mzee Mwinyi na yeye alimsamehe, lakini Ibrahim ameshitakiwa na Jamhuri wala si mzee Mwinyi.

"Malalamiko na maombi yake kuhusu mateso anayoyapata mwanaye, mimi nitayachukua na kuyafikisha kwa Rais Kikwete na Mzee Mwinyi ili aweze kutendewa haki huko aliko,” alisema Mufti Simba.

Afisa Uhusiano wa Magereza, Omar Mtiga alisema hana taarifa juu ya madai hayo na kuahidi kuwa apewe muda kidogo ili awasiliane na watu walioko gerezani ambao ndio wanaokaa na mfungwa huyo.

“Mimi sipo gerezani leo, ngoja niwasiliane na wanaokaa naye halafu nitakupigia,” aliahidi Mtiga.

Alipotafutwa tena alisema, “Kwani wewe umesikia nini?” alihoji na kujibiwa kuelezwa malalamiko ya mzazi wa Said. Alijibu kwa ufupi “Ahh! Na kuhoji, kwani wewe umeambiwa yupo gereza gani?” alijibiwa na mwandishi, Keko, alikaa kimya kidogo na baadaye kusema “Ok, ngoja niwapigie nilikuwa nawapigia siwapati. Nitakujulisha” alijibu Mtiga.

Hadi tunakwenda mitamboni afisa huyo hakuwa amepatikana. Wakati huo huo, Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu (T), limemtaka Mzee Mwinyi kumtoa gerezani kijana huyo aliyefungwa mwaka mmoja kwa kosa la kumshambulia Mwinyi kwa madai kuwa ndiye alimpandisha hasira kwa kuwashawishi Waislamu kutumia kondomu.

Aidha, Baraza hilo limezindua rasmi mfuko maalum wa kumsaidia na familia yake katika kipindi chote cha mwaka mmoja wa kifungo hicho, na Sh600,000 zilikusanya papo hapo.

Tamko hilo lilitolewa katika Baraza la Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) lililoandaliwa na baraza hilo na kufanyika juzi ndani ya Msikiti wa Kituo cha Kiislamu Tanzania (TIC) Magomeni jijini Dar es Salaam.

Akisoma maazimio ya baraza hilo yaliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, msemaji wa baraza hilo, Sheikh Salim Khator alisema Mwinyi ana wajibu wa kumtoa gerezani kijana huyo kwa kuwa yeye ndiye alisababisha kifungo chake.

Alisema suala la Waislamu kumsaidia mwenzao aliyepata matatizo ni la lazima na hivyo, wote wanapaswa kuwasilisha michango yao katika ofisi za baraza hilo kwa ajili ya kijana huyo.

“Tunazindua rasmi mfuko maalumu utakaotumika kumuhudumia ustadhi Ibrahim na familia yake iliyobaki nyumbani,” alisema Khator.

Alisisitiza kuwa Waislamu kwa nafasi zao wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanaenda mahakamani kumtembelea na kumsaidia Ibrahim kwa hali na mali kwa kuwa huo ndio wajibu wao.

“Tunasisitiza kuwa msimamo wetu wa miaka yote ni kumsaidia Muislamu yoyote atakayepata matatizo akiutetea uislamu.

Waislamu watamtetea na kumsaidia kwa hali na mali bila kumuogopa yeyote,” alisema Khator.

“Tunalaani kitendo cha jeshi la polisi kumtisha na kumkamata Shafiq Rashid kwa kuonyesha nia yake njema ya kumsaidia ustadhi Ibrahim Said,” alisema.

Tamko hilo liliitaka Bakwata kuwaomba radhi Waislamu kwa kuandaa mazingira yaliyosababisha tukio la kuchapwa Mwinyi na hatimaye kifungo kwa ustadhi Said.

Hata hivyo, Mufti ambaye alikwishaomba radhi siku ya tukio, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa hajapata nakala rasmi ya tamko hilo la jumuiya hiyo.

Alieleza kuwa msimamo wa uislamu kuhusu kondomu ni suala linalojadilika kwa wanandoa, lakini kwa waliokuwa hawajaoa au kuolewa ni haramu kuitumia.

Machi 9 mwaka huu, Mwinyi alijikuta anashambuliwa kwa kibao na kijana Said, baada ya kujaribu kuwashawishi Waislamu kutumia kondomu wanaposhindwa kujizuia.


Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment