Sunday, March 8, 2009

Maximo akata mzizi wa fitina Stars, awatema rasmi Boban na Chuji

Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania, taifa Stars Marcio maximo akizungumza na waandishi wa habari wakati alipotangaza timu yake jana.

KOCHA wa Taifa Stars, Marcio Maximo amewaita wachezaji wapya watano katika kikosi chake ambacho hakijumuishi wachezaji wote wa Yanga.

Katika kikosi hicho, kiungo wa Simba, Haruna Moshi 'Boban' na kipa Farouk Ramadhan wa Miembeni wameachwa.

Akitangaza kikosi hicho jana, Maximo alisema ni kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa Amerika Kaskazini, Vancouver Whitecaps ya Canada katika mechi itakayochezwa Machi 14 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pia, kocha huyo alisema ameamua kuwaacha wachezaji wote wa Yanga kwa kuwa wanajiandaa na mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya watetezi, Al Ahly ya Misri itakayochezwa Machi 15 mjini Cairo.

Kikosi kamili cha Stars kinaundwa na makipa: Shaban Dihile (JKT), Deogratius Mushi ' Dida' ( Simba), Eddy Bushiri ( JKU Zanzibar).

Mabeki: Erasto Nyoni ( Azam), Salum Swed ( Mtibwa), Kelvin Yondan , David Naftari, Juma Jabu ( Simba), George Minja ( JKT) na Stephano Mwasika ( Moro United). Viungo: Henry Joseph, Jabir Aziz ( Simba), Shaban Nditi ( Mtibwa), Nizar Khalfan ( Moro), Mwinyi Kazimoto ( JKT).

Washambuliaji: Mussa Mgosi ( Simba), Zahoro Pazi, Uhuru Suleiman ( Mtibwa) na John Bocco ( Azzam). Pia, kocha huyo amewaita vijana chini ya miaka 20 ambao ni Razak Khalfan ( Yanga), Khalid Haji, Furaha Yahaya ( JKT), Haji Ally Nuru na Ahmed Hassan kutoka kwa Kipingu Academia.

Kuhusu suala la viungo wawili waliokuwa Stars, Haruna Moshi ' Boban' na Athuman Idd 'Chuji; pamoja na beki Amir Maftah wa Yanga ambao wanadai kuachwa, alieleza kuwa wamekuwa watovu wakubwa wa nidhamu, wasiofuata ratiba tangu wakiwa nchini na ugenini licha ya kuwakanya, lakini walishindwa kubadilika.

'' Mimi nataka wachezaji wenye nidhamu na ambao watanielewa ili tuweze kufanikiwa na kufanya vizuri, lakini Boban na Chuji, wao ni watovu wa nidhamu wako kinyume na ratiba yangu, hawataki kufanya mazoezi, lakini wanataka kupangwa kwenye mechi kitu ambacho hakiwezekani, '' alisema Maximo.

Aliongeza kuwa kutokana na hilo ameufunga rasmi mjadala huo na hataki kulizungumzia tena suala lao.

Akitoa tathmini ya michuano ya CHAN, Maximo alisema wachezaji wake walijitahidi kupigana kama alivyosema mwanzo kuwa wanakwenda vitani ili wapate ushindi na si kuwakilisha.

Alisema vijana wake walionyesha kuwa kweli walipambana kwa kucheza vizuri na hata kuifunga timu kubwa Afrika, Ivory Coast.

Alisema japo walitolewa mapema, lakini walionekana kuwa walikuwa na nia ya kuendelea na walitolewa wakiwa na pointi nne, kitu ambacho kimewapa matumaini makubwa.

Aliwataja wachezaji ambao walimfurahisha kwa uchezaji wao katika mashindano hayo kuwa ni Mussa Hassan Mgosi, Salum Swed na nahodha Shadrack Nsajigwa.

Alisema kikosi alichokichagua safari hii amezingatia sana uwezo wa mchezaji, umri, nidhamu na uzalendo.

''Ningependa sana timu yangu iwe na vijana wengi kwa ajili ya kuwajenga na kuwaandaa kwa baadaye kwani wachezaji wengi wa Stars wa sasa umri wao umeisha'' alisema Maximo.

Alisema wachezaji hao wataingia kambini jumanne tayari kwa ajili ya maandalizi ya mechi hiyo ila wachezaji wa Simba wanaripoti kambini siku ya jumatano baada ya kumaliza mechi yao na Vancouver.


Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment