Friday, March 6, 2009

Mwakilishi CUF Ajiuzulu Kwa Kashfa

MWENYEKITI wa Kamati ya Kuchunguza Mahesabu ya Fedha na Uchumi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), katika baraza la wawakilishi (PAC), Abass Juma Mhunzi ametangaza rasmi kujiuzulu wadhifa huo.

Mhunzi, ambaye ni mwakilishi wa Jimbo la Chambani kwa tiketi ya CUF, alisema kuwa amemwandikia kiongozi wa upinzani kumjulisha kuhusu uamuzi wake kutokana na spika wa Baraza la Wawakilishi kutokuwepo kisiwani hapa kwa sasa.

Mhunzi alirushiwa tuhuma nyingi, zikiwemo za kushindwa kununua magari ya wawakilishi wenzake baada ya kupewa karibu Sh72 milioni, lakini aliiambia Mwananchi jana kuwa magari hayo yamechelewa kufika na kwamba endapo hayatafika, yuko tayari kuuza mali zake kufidia fedha hizo ambazo alipewa na wajumbe wenzake.

"Kuhusu wajumbe kunipa fedha kwa ajili ya kununulia magari, ni kweli na hayo magari yamechelewa. Yanakuja, lakini nikishindwa nitawalipa hata kwa kuuza mali zangu," alisema Mhunzi kwa njia ya simu alipozungumza na Mwananchi.

Mhunzi amepata umaarufu mkubwa katika vikao vya baraza la wawakilishi kutokana na misimamo yake ya kutetea matumizi mabaya ya fedha za serikali.

Katika kipindi chake cha uwakilishi, aliwahi kukumbana na matatizo mengi, likiwemo la kufikishana mahakamani na spika wa baraza hilo, Pandu Ameir Kificho baada ya kupewa adhabu ya kutohudhuria katika vikao kwa mwaka mzima.

Adhabu hiyo ilitolewa baada ya Mhunzi kukataa kuomba radhi baraza kutokana na matamshi yake ya kusema bei za mafuta zinapangwa Ikulu.

Katika kadhia hiyo Spika kificho alimuamuru Mhunzi kutohudhuria vikao kwa mwaka mzima, lakini mwakilishi huyo alipinga mahakamani na kushinda kesi na kulipwa haki yake kwa mwaka mzima.

Mwaka jana, Mhunzi pia aliwataka wawakilishi wenzake wa kambi ya upinzani kubadili mwelekeo na kuitambua SMZ iliyo chini ya Rais Amani Abeid Karume.

Mhunzi alisema kwamba anajua kwamba msimamo wake huo unaweza ukawa mwisho wake katika duru za kisiasa na kummaliza, lakini aliwataka wenzake kufahamu ukweli huo na kinachofanyika ni mbwembwe tu za kisiasa huku akisisitiza kuwa Rais Karume ndiye kiongozi wa nchi.

Kujiuzulu kwa Mhunzi kumekuja siku chache baada ya baraza kuu la uongozi la chama chake cha CUF kumbwaga katika nafasi yake ya mjumbe wa baraza hilo. Uchaguzi huo ulifanyika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Awali jana, akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Baraza la Wawakilishi zilizo Maisara mjini hapa, kiongozi wa kambi ya upinzani kwenye baraza la wawakilishi, Abubakar Khamis Bakari alisema Mhunzi anashutumiwa kutumia fedha kifisadi na anadaiwa kuchota zaidi ya Sh200 millioni ambazo inadaiwa zilitengwa kwa ajili ya kununulia magari wajumbe wenzake.

Bakari alisema mwakilishi huyo anadaiwa kuchukuwa fedha hizo kwa ajili ya kutafuta magari kwa wajumbe wa baraza la wawakilishi na fedha za michango ya wajumbe wa baraza hilo wa kambi ya upinzani.
Kiongozi huyo alisema Mhunzi alipewa kiasi cha Sh72 milioni tangu mwaka 2006 kwa ajili ya kununua magari ya wawakilishi wenzake, lakini hadi sasa ameshindwa kufanya kazi hiyo wala kurejesha fedha alizopewa.
Alisema pia Mhunzi anadaiwa kushindwa kufikisha hundi 21 kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na nyingine 39 kwenye Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), ambazo ni kwa ajili ya shughuli hiyo.

Kiongozi huyo amesema fedha hizo zilikuwa ni mchango wa wajumbe wa baraza la wawakilishi ambao walikuwa wakikatwa katika mishaha yao kwa ajili ya kusaidia matatizo mbali mbali yanayoweza kutokea katika kipindi chao chote cha shughuli za baraza hilo.

Kiongozi huyo wa upinzani amesema kunatokana na kashfa kubwa zinazomkabili za upotevu wa mamilioni ya fedha pamoja na utapeli aliokuwa akiufanya kwa muda mrefu.

Bakari alisema tayari Mhunzi ameshamuandikia barua Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho pamoja na kiongozi wa kambi ya upinzani kueleza uamuzi huo.

"Ameniandikia kwa kuwa mimi ni kiongozi wa kambi ya upinzani na katika barua yake ameainisha baadhi ya vitisho, akisema anakusudia kunimaliza kisiasa," alisema Bakari ambaye ni mwakilishi wa Jimbo la Mgogoni kisiwani Pemba.

Pia katika barua yake Mwakilishi huyo ilisema anakusudia kufanya jambo kubwa kabisa ambalo litaitetemesha nchi na upinzani kupata pigo la mwaka.


No comments:

Post a Comment