Sunday, April 5, 2009

Yanga nje Kombe la Afrika baada ya kupigwa na Al Ahly Dar

NI dhahiri mashabiki wa Yanga walikuwa wanalitambua kwamba timu yao haiwezi kushinda, mabao 4-0 lakini walichokifuata ni kuona aina ya soka ya Al Ahly na nyota wake.

Al Ahly iliifunga Yanga mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika mjini Cairo, ikaifunga tena bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana ikiwa ni mchezo wa marudiano.

Yanga ambayo iliweka rekodi kwa kuitoa Etoile d’Or Mirontsy ya Comoro kwa mabao 14-1 walishindwa kabisa kuonyesha soka yao halisi huku Al Ahly wakionana karibu kila idara katika vipindi vyote.

Aliyewakatisha tamaa Yanga alikuwa Flavio Amado aliyefunga bao pekee katika dakika ya tano baada ya mabeki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Shadrack Nsajigwa na Wisdom Ndhlovu kujichanganya na mpira kumkuta mfungaji aliyeukwamisha wavuni kirahisi.

Katika mchezo huo ambao ulianza kwa kukumbuka mashabiki 22 waliokufa uwanjani Ivory Coast, Yanga ilianza kwa matumaini lakini wakati wakielekeza mashambulizi, Shadi Mohamed wa Al Ahly aliunasa na kutoa mpira kwa Mohamed Barakat ambaye naye aliwachanganya wachezaji wa Yanga na kumkuta Flavio.

Yanga waliokuwa wakiongozwa na Athumani Idd ‘Chuji’, Mrisho Ngassa, Mick Barasa na Abdi Kassim walijaribu kuipenya ngome ya Ahly lakini ukuta wake chini ya Ahrd Sayed, Gipergo Sebastian, Wae Gomaa na Shadi walisimama imara na kuyadhibiti mashabulizi ya Yanga.

Katika dakika ya 17, Al Ahly waliokuwa wakicheza pasi fupifupi za uhakika ambazo mashabiki wa Simba walikuwa wakizihesabu mara kwa mara hadi 10 kabla ya kupotea, walifanya mashambulizi ya kushtukiza lakini yasiyo na faida.

Mohamed Aboutrika alifunga bao katika dakika ya 20, lakini mwamuzi alilikataa kwa madai mfungaji alikuwa ameotea.

Kipindi cha pili, Yanga ilianza kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza kwa mashambulizi mfululizo, lakini kibao kiligeuka kwa wageni waliokuwa wakicheza 3-5-2 na wakati mwingine 4-4-2 kuonana kwa pasi fupi fupi za haraka katika dakika ya 48, 50 na 54.

Yanga wakitumia mfumo wa 4-4-2 walijibu kwa shambulizia kali na kupata kona tatu mfululizo katika dakika za 55, 56 na 57 lakini walikosa umakini na kupoteza mpira.

Hata hivyo pamoja na kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Abdi Kassim, Boniface Ambani na Barasa na nafasi zao kuchukuliwa na Shamte Ally, Ben Mwalala na Jerry Tegete lakini hawakuweza kubadili sura ya mchezo.

Kocha wa Yanga, Dusan Kondic baada ya mchezo huo alisema: “Tumefungwa kutokana na makosa ya ngome, wenzetu walitumia nafasi hiyo kufunga.

Sisi tumetengeneza nafasi nyingi lakini tumeshindwa kufunga. “Nawapongeza Al Ahly, ni timu nzuri, ina kila sababu za kushinda kwa kuwa wamekaa pamoja muda mrefu, wana uzoefu na wana kila sababu ya kushinda.

Binafsi nawapongeza wachezaji wangu licha ya kutolewa kwa kweli wamejitahidi.

Akizidi kuisifu Al Ahly alitoa mfano kwa kusema msimu uliopita waliifunga Enyimba ya Nigeria mabao 6-1 lakini wakafungwa 2-1 mjini Aba, Nigeria.

“Enyimba ni timu ngumu, ni timu kali Afrika lakini walipigwa hayo tofauti na sisi…nawapongeza sana Al Ahly.”

Kocha huyo alisema kuwa Yanga inaweza kufanya vizuri baada ya miaka mitatu: “wakati naingia Yanga, nilisema mafanikio yangu ni baada ya miaka mitatu, sasa nina mwaka mmoja, baada ya miaka mingine miwili, mtaiona Yanga.”

Kocha wa Al Ahly, Manuel Josse alikataa kuzungumzia mchezo huo.Timu hiyo iliondoka jana jioni kurudi nyumbani ikipitia Nairobi.

Yanga iliwakilishwa na: Kaseja, Nsajigwa, Nurdin, Haroub, Ndhlovu, Owino, Ngassa, Abdi/Shamte Ally, Idd, Ambani/Mwalala, Barasa/Tegete.


Source: Mwananchi



No comments:

Post a Comment