Thursday, April 2, 2009

Meli yazua kasheshe kwa wakazi Kigamboni

Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam wakiishangaa meli ya mizigo ambayo imekwama kuanzia Jumanne ufukweni karibu na Bandari ya Dar es Salam. Juhudi za kuikwamua zilikuwa bado zinaendelea Jumatano

WAKAZI wa Kigamboni jijini Dar es Salaam jana walikumbuka kwa muda adha ya usafiri wa kivuko baada ya meli ya mizigo ya MSC FEDERICH kukwama kwenye njia ambayo kivuko cha Mv Magogoni hupitia kuvusha abiria na mizigo.

Meli hiyo ilikwama kwa masaa kadhaa kabla ya boti kuivutia kando kidogo kwa njia hiyo na hivyo kukipa mwanya kivuko hicho kuendelea na kazi ya kuvusha watu.

Habari ambazo Mwananchi ilizipata kutoka eneo la tukio zinasema kuwa nahodha wa meli hiyo alipoteza mawasiliano na chombo kilichokuwa kikiiongoza na hivyo kwenda nje ya njia yake na kukwama.

Kazi ya kuivuta meli hiyo ilionekana kuwa ngumu kutokana na minyororo iliyotumiwa na boti hizo tatu ndogo kukatika mara kwa mara na kuwapa kazi kubwa mabaharia kufunga tena na kuendelea kuivuta.

Hadi tunaenda mitamboni, boti hizo tatu zilishindwa kuiondoa kabisa meli hiyo na kurudi kwenye maegesho yao, lakini kivuko kiliendelea na shughuli zake za kuvusha abiria na mali.

Wakazi wa Kigamboni wamekuwa waathirika wakubwa wa tatizo la kivuko na mara kadhaa wamejikuta wakilazimika kusubiri kwa muda mrefu; kutumia boti ndogo au kuzunguka kwa barabara kupitia Mbagala ili kurudi au kwenda Kigamboni.

Lakini mwishoni mwa mwaka jana, wakazi wa Kigamboni walipata suluhisho la matatizo yao baada ya kivuko cha Mv Magogoni kujengwa na hawajawahi kupata tatizo la usafiri katika siku za karibuni.


Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment