Saturday, April 25, 2009

Mamia ya mashabiki wa soka wamzika golikipa wa zamani Sahau Kambi

MAMIA ya wapenzi na mashabiki wa soka wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe pamoja wachezaji wa soka wazamani jana walifurika katika makaburi ya Tandika Mikoroshini katika mazishi ya mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Sahau Kambi.

Kambi alifariki dunia Jumanne Aprili 21 baada ya kusumbuliwa na matatizo ya tumbo pamoja na kisukari.

Wakizungumza na Mwananchi jana baadhi ya wachezaji wa zamani waliowahi kucheza naye soka mara baada ya kumalizika kwa mazishi walisema kuwa Tanzania imepoteza mtu muhimu katika michezo.

"Tumepoteza mtu muhimu katika michezo, kwani marehemu ni miongoni mwa Watanzania wachache waliotoa mchango mkubwa katika kuhakisha Tanzania inapiga hatua mbele zaidi katika soka.

"Lakini kwa vile imeisha tokea hatuna budi kumwombea kwa Mwenyezi Mungu na kuyaenzi mazuri yote aliyoyatenda enzi za uhai wake,"walisema wachezaji hao Zamoyoni Mogela, Gebo Peter, Dua Saidi, Abeid Mziba, Abeid Kasabalala, Ken Mkapa, Felix Minziro na Steven Nemes kwa hakika walionekana kuguswa sana na msiba huo.

Nao baadhi ya wapenzi na mashabiki wa soka waliohudhuria mazishi hayo walieleza kuwa watamkumbuka mlinda mlango huyo kutokana na uhodari wake na kupewa jina la 'Tanzania One' katika miaka ya 1990 akiwa na timu ya Yanga.

Mashabiki wa Yanga wanamkumbuka Sahau Kambi kwa kitendo chake cha kumrudishia mpira mshambuliaji wa Simba marehemu Edward Chumila aliyefunga bao lililopekea Fred Felix Miziro kocha wa Moro United kuanza kupiga, 'Sahau ata sahau'.

Kambi baada ya kuachana na soka alikuwa mshauri wa Balozi wa Comoro nchini na kazi aliyokuwa akifanya mpaka anafariki Dunia, hivi karibuni alikuwa mdhamini wa Mkurugenzi wa Zamani wa timu ya Moro United, Merey Balhabou anayekabiliwa na kesi ya kujipatia fedha isivyo halali katika benki ya Barclays.

Mungu aweke roho ya marehemu mahali pema peponi, Amen.



Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment