Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Vicky Ntetema akiwa mjini Dar es Salaam mamia ya watu wamejeruhiwa wakati wakikimbia kwa hofu wakati milipuko hiyo ilipokuwa ikiendelea kurindima.
Polisi wamesema majengo kadha katika eneo la tukio yaliungua moto kutokana na vipande vya mabomu yaliyokuwa yakipaa hewani katika ghala la silaha la jeshi la Mbagala.
Mitikisiko ya takriban milipuko mitatu ilisikika katika maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam ambapo maofisa wa serikali waliwashauri wafanyakazi kuondoka katika majengo yao ya kazi.
Watu wengi walikuwa na hofu kubwa huenda ni mashambulio ya mabomu kama yaliyotokea mwaka 1998 yakihusishwa na kundi la al Qaeda, ambayo yalileta kizaazaa katika jiji la Dar es Salaam.
Ghala hilo la jeshi likiwa jirani na kambi ya jeshi kilometa 14 nje ya katikati ya jiji la Dar es Salaam, inaaminika linahifadhi kiasi kikubwa cha silaha yakiwemo mabomu na makombora yanayotumika katika mizinga.
Mwandishi wa BBC anasema hospitali ya karibu ya Temeke ilihemewa na majeruhi na inaaminika idadi ya vifo huenda ikaongezeka.
Eneo lililoathirika na kuangukiwa na vipande vya mabomu hayo ni kubwa.
Mwandishi wetu Vicky Ntetema amesema alishuhudia mabaki ya mabomu hayo pamoja na mwili wa mtu aliyeuawa kiasi cha kilometa 15 kutoka kambi ya jeshi.
Karibu na eneo lililotokea milipuko, afisa mmoja mwandamizi wa polisi Paul Chagonja amesema wamepokea taarifa zisizothibitishwa kwamba baadhi ya watoto walizama baada ya kuingia mtoni wakiwa wanakimbia kutokana na hofu ya milipuko.
Amesema idadi kubwa ya nyumba zimehariwa katika eneo hilo, nyingine zikiwa zimepata nyufa kubwa huku baadhi zikiwa zimebomoka kabisa.
Source: BBC
No comments:
Post a Comment