Monday, April 20, 2009

Simba, Yanga ngoma nzito zatoka sare ya 2-2

Kelvin Yondan wa timu ya Simba akichuana na washambuliaji wa timu ya Yanga Ben Mwalala (Chini) na Boniface Ambani katika mechi ya ligi kuu Tanzania bara kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam jana.Matokeo 2-2

MSHAMBULIAJI Jerry Tegete alizima kelele na shangwe za mashabiki wa Simba kwa kufunga bao la kusawazisha katika dakika za nyongeza kufanya
matokeo 2-2 kwenye mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.


Mashabiki wa Simba walikuwa wakishangilia kipindi chote cha mchezo furaha yao ilizidi baada ya winga wake Ramadhani Chombo 'Redondo' kuunganisha kwa kichwa krosi ya Henry Joseph dakika ya 23 kuandika bao la kwanza kwa wekundu hao.

Kuingia kwa bao hilo kuliamsha ari kwa timu ya Simba kufanya mashambulizi hadi mapumziko walikuwa wakioongoza kwa bao 1-0.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya, Ben Mwalala aliisawazishia Yanga katika dakika ya 48 na kukimbilia eneo walipo mashabiki wa Simba na kuwafunga mdomo kitendo kilichowakera na kuanza kurusha chupa za maji.

Hata hivyo dakika ya 62, mchezaji bora wa mechi hiyo Haruna Moshi 'Boban' aliifungia timu yake bao la pili baada ya kuuwahi mpira uliopanguliwa na kipa Juma Kaseja likiwa shuti la Ramadhani Chombo.

Kiungo Haruna Moshi alionyesha mchango mkubwa kwa timu yake jambo lilopelekea jopo la ufundi kumtangaza mchezaji bora wa mechi na kuzawadiwa shilingi 300,000 .

Bao hilo la Boban lilidumu hadi dakika 90 kabla ya Jerry Tegete kuzima furaha za mashabiki wa Simba baada ya kuunganisha krosi ya Mike Barasa kwa kifua na kumwacha kipa wa Simba, Ally Mustapha asijue la kufanya.

Katika mchezo huo ulishuhudia timu zote zikicheza soka safi na kukamiana,huku Yanga wakitumia zaidi mipira ya krosi na washambuliaji wake warefu Ben Mwalala, na Boniface Ambani kupiga vichwa na kuwapa wakati mgumu mabeki wa Simba.

Mashabiki walifurahi zaidi soka ya upinzani iliyoonyesha kati ya Haruna Moshi na Nadir Haroub huku kwenye nafasi ya kiungo kulikuwa na kazi kubwa kati ya Henry Joseph, Niko Nyagawa na Ramadhani Chombo wa Simba dhidi ya Godfey Bonny, Nurdin Bakari na Mike Baraza kufanya mwamuzi kuwa na wakati ngumu.

Viatu, kusukumana na maneno ya hapa na pale baina ya wachezaji yalisababisha mwamuzi Israel Nkongo kutoa kadi za njano kutuliza hali ya mchezo.

Mwamuzi wa mchezo huo Israel Nkongo alilalamikiwa na mashabiki wa timu zote mbili kwa kutoa kadi nyingi za njano kabla ya kumtoa kwa kadi nyekundu mchezaji Nadir Haroub 'Cannavaro'. Nadir Cannavaro alizawadiwa kadi hiyo baada ya kuvua jezi wakati timu yake iliposawazisha, awali alilimwa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Ramadhani Chombo.

Tofauti na siku za nyuma mechi za watani hao zimekuwa zikigubikwa na imani za kishirikina, mechi ya jana hakukuwa na vitendo hivyo na wachezaji walionyesha mpira ni furaha na si uhasama baada ya kubadilisha jezi mara baada ya mchezo.

Kabla ya mchezo mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali aliingia uwanjani na kuonyesha ishara ya vidole vitatu akimanisha magoli matatu, lakini mambo hayakuwa alivyotegemea.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo kocha wa Simba, Mzambia Patrick Phiri alisema "Yanga imebadilika tofauti na siku za nyuma, ni timu imara ina wachezaji wazuri, matokeo ya leo si mazuri kwetu kwa vile tulishakuwa washindi tumepoteza dakika za mwisho,"alisema Phiri.

Wakati Phiri akisema hayo, kocha wa Yanga, Dusan Kondic alipompongeza Mzambia Patric Phiri kwa kuibadilisha Simba na kuifanya icheze kitimu tofauti na ilivyokuwa katika mchezo wa awali.

"Nina furaha kwa matokeo haya, timu zote zimecheza mpira mzuri mabadiliko yaliyofanywa na timu zote ni mazuri mwamuzi kwa upande wangu ni mzuri,"alisema Kondic ambaye pia alilalamikia kitendo cha baadhi ya wapenzi wa Yanga ambao wamekuwa wakimtuhumu yeye na Obren kuwa anaiharibu Yanga na kudai kamwe hawezi kununua mchezo na badala yake anataka mpira uchezwe uwanjani.



Source: Mwananchi.

No comments:

Post a Comment