Sunday, November 30, 2008

Taifa Stars yaifunga Sudan 3-1

TIMU ya soka ya Tanzania, Taifa Stars jana iliikandamiza Sudan ‘Mwewe wa Jangwani’ kwa mabao 3-1 katika mechi ya kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani (CHAN).

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa, Dar es Salaam, Stars iliandika bao lake la kwanza katika dakika ya 20 lililofungwa kwa shuti kali na Jerry Tegete baada ya kuinasa pasi ya Mrisho Ngassa.

Hata hivyo furaha ya mashabiki wa Stars ilizimwa ndani ya dakika mbili tu baada ya kupata bao la kuongoza, baada ya Badreldin Eldod kupiga kona iliyotua kichwani kwa Seifdin Ali Idrisa aliyezitingisha nyavu za Stars na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Stars iliandika bao la pili katika dakika ya 60 mfungaji akiwa ni Athuman Idd ‘Chuji’. Chuji alifunga bao hilo kwa shuti la umbali wa mita 30 na hivyo kurudisha matumaini ya Stars ambayo tayari ilikuwa imeonyesha uhai.

Juhudi za Stars zilizoandamana na pasi safi za uhakika zaidi ya 15 ziliiwezesha kuandika bao la tatu lililofungwa na Kiggi Makassy, bao lililoamsha shangwe na vigelegele kwa mashabiki ambao ni dhahiri walifurahishwa na umakini ulioonyeshwa hadi kupatikana kwa bao hilo.

Mabao hayo hayakuwa mwisho wa Stars kuiandama Sudan, mara kadhaa timu hiyo ilifanya mashambulizi na mfano ni mabao mawili yaliyofungwa na Ngassa ambayo mwamuzi, Mnkantjo Ntaban wa Zimbawe aliyakataa kwa madai kwamba mchezaji huyo aliotea.

Dakika ya 88 Sudan ilijikuta ikimpoteza kipa wao, Akram Elhad ambaye alipewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Ngassa wakati akienda kufunga.

Baada ya kipa huyo kutolewa Sudan ililazimika kumvisha glovu mchezaji wake wa ndani, Mudather Eltaib na kumuweka golini baada ya kuwa wamemaliza idadi ya wachezaji watatu wa kubadilishwa.

Stars ambayo tayari imefanikiwa kuzitoa Kenya na Uganda katika kinyang’anyiro cha kusaka tiketi ya michuano hiyo, sasa inahitaji sare ya aina yoyote au kutofungwa zaidi ya bao moja ili iweze kusonga mbele na kushiriki fainali za michuano hiyo zitakazochezwa Ivory Coast hapo mwakani.

Stars: Shaaban Dihile, Shedrack Nsajigwa, Juma Jabu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ Salum Swedi ‘Kussi’, Geoffrey Bonny, Henry Joseph/Kiggi Makasy, Athuman Idd/Nurdin Bakar, Jerry Tegete/Mussa Hassan ‘Mgosi’, Haruna Moshi na Mrisho Ngassa.

Sudan: Akram Elhad, Ritshard Jasten/Khalid Hassan, Mohamed Ali lakhidir, Amir Damar Kuku, Nasredin Omer, Saifeldin Ali Idris, Mohamed Tahir, Badreldin Eldod, Balla Gabir/Tariq Mukhtar, Haitham Kamal na Mudather Eltaib/Abdelhamid Amar.

2 comments:

  1. Good job lkn embu rekebisha basi hiyo setting yako basi,post mojamoja inachosha Mzee

    ReplyDelete
  2. Ok thanks Anselm..lakini kwenye setting kuko sawa sema upatikanaji wa news ndio tatizo si unajuwa mambo yenyewe najaribu tu wala sio fani yangu..kwa hiyo kama utakuwa na news unaweza kunitumia na mimi nitaziweka bila tatizo.

    ReplyDelete