skip to main |
skip to sidebar
WADHAMINI wa timu ya soka ya taifa (Taifa Stars), Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) imetoa motisha ya Sh milioni moja kwa kila mchezaji na viongozi wa benchi la ufundi la timu hiyo endapo itaibuka na ushindi katika mchezo wa dhidi ya Sudan hapo kesho jioni.
Stars kesho jioni itacheza na Sudan katika Uwanja Mkuu wa taifa kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani ambapo mchezo wa marudiano umepangwa kufanyika wiki mbili zijazo mjini Khartoum Sudan.
Akizungumza mjini Dar es Salaam, Meneja Mawasialino na Uhusiano wa SBL, Teddy Mapunda alisema kuwa baada ya mchezo huo kama Stars itashinda itafanyika sherehe ya kuwapongaza wachezaji sambamba na kukabidhiwa fedha zao.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Muhammed Seif Khatib amewataka wachezaji wa timu ya soka ya taifa (Taifa Stars) kucheza kwa kujiamini ili kuhakikisha inakata tiketi na kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani.
Alisema kuwa wachezaji wanatakiwa wasikate tamaa baada ya kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini mwaka 2010 na Mataifa ya Afrika mwaka huo nchini Angola.
Alisema kuwa Stars ina uwezo wa kusonga mbele kwa kuwa soka la Tanzania limepiga hatua kubwa na kuongeza kwamba nafasi pekee iliyobaki ni kuhakikisha inashinda mchezo wa leo.
Khatib aliongeza kuwa kupungua kwa migogoro ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na juhudi za serikali kuwekeza kwa makocha, ufundi na viwanja kumesaidia kwa kiasi kikubwa kukuza mchezo wa soka nchini.
“Sasa Watanzania wanataka ushindi wamechoka kushindwa mara kwa mara wakati mchezo huu unaonekana kukua kwa kiasi kikubwa tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma,” alisema.
Aidha, Khatib aliwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete za kuitakia timu hiyo ushindi katika mchezo wa kesho.
No comments:
Post a Comment