Monday, May 25, 2009

Mahakama Yamsafisha Snoop


CALIFORNIA, Marekani
BAADA ya Mahakama ya Santa Monica kumsafisha Snoop Dogg kwamba hakumpiga shabiki aliyemfungulia kesi na kudai fidia, mwanamuziki huyo ameamua kuongeza ulinzi katika maonyesho yake.

Mkali huyo wa miondoko ya hip hop, amechukua uamuzi huo ili kuepukana na matukio ambayo ameyatafsiri na watu wengi yanaweza kuwa wanayafanya kwa lengo la kujifaidisha kupitia yeye.

Shabiki Richard Monroe Jr aliiambia mahakama kuwa Snoop alimpiga na kipaza sauti usoni baada ya kupanda jukwaani, hivyo kutaka alipwe fidia ya dola milioni 22.

Hata hivyo baada ya ushahidi wa mkanda wa video kutumika ikabainika Snoop hakufanya hivyo badala yake, kampuni yake ya Doggy Style ilitakiwa kumlipa shabiki huyo fidia ya dola 295,950.

Monroe Jr aliiambia mahakama alipanda jukwaani baada ya Snoop kuwaalika mashabiki jukwaani wakati akiimba singo yake maarufu ya Gin en Juice lakini alishangaa kukutana na kipigo kikali cha kushitukiza.

Hata hivyo, Snoop alikanusha madai ya kumshambulia mtu huyo na ushahidi wa video ulithibitisha na kumuondoa matatizoni.



Source: Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment