Monday, May 25, 2009

Mahakama Yamsafisha Snoop


CALIFORNIA, Marekani
BAADA ya Mahakama ya Santa Monica kumsafisha Snoop Dogg kwamba hakumpiga shabiki aliyemfungulia kesi na kudai fidia, mwanamuziki huyo ameamua kuongeza ulinzi katika maonyesho yake.

Mkali huyo wa miondoko ya hip hop, amechukua uamuzi huo ili kuepukana na matukio ambayo ameyatafsiri na watu wengi yanaweza kuwa wanayafanya kwa lengo la kujifaidisha kupitia yeye.

Shabiki Richard Monroe Jr aliiambia mahakama kuwa Snoop alimpiga na kipaza sauti usoni baada ya kupanda jukwaani, hivyo kutaka alipwe fidia ya dola milioni 22.

Hata hivyo baada ya ushahidi wa mkanda wa video kutumika ikabainika Snoop hakufanya hivyo badala yake, kampuni yake ya Doggy Style ilitakiwa kumlipa shabiki huyo fidia ya dola 295,950.

Monroe Jr aliiambia mahakama alipanda jukwaani baada ya Snoop kuwaalika mashabiki jukwaani wakati akiimba singo yake maarufu ya Gin en Juice lakini alishangaa kukutana na kipigo kikali cha kushitukiza.

Hata hivyo, Snoop alikanusha madai ya kumshambulia mtu huyo na ushahidi wa video ulithibitisha na kumuondoa matatizoni.



Source: Mwanaspoti

Sasa waukataa uharamia Somalia

Kukosekana serikali thabiti nchini Somalia kwasababisha uharamia kustawi

Baada ya kuonekana ni tatizo kubwa Pembe ya Afrika, maharamia wapatao 200 wa Kisomali wametangaza kuacha shughuli hiyo katika mkutano uliofanyika kaskazini mwa nchi hiyo.

Wanachama wa makundi ya maharamia walikutana na viongozi wa mabaraza ya wazeee na wataalam wa Kisomali katika mji wa Eyl, katika jimbo lililojitangazia uhuru la Puntland na wakaahidi kusimamisha mara moja utekaji nyara wa meli.

Mwakilishi wa maharamia hao Abshir Abdullah ameiambia BBC kwamba wataziachilia meli zote wanazoshikilia na watawaachilia huru mabaharia wanaowashikilia .

Maharamia wamekuwa katika chagizo kubwa kutoka kwa wazee wa Kisomali, waliokuwa wakiwashutumu kwa kuiaibisha jamii yao.

Tangu mwaka 1991 Somalia imekuwa haina serikali thabiti hali iliyofanya uharamia ustawi.

Licha ya manowari za kijeshi za kimataifa kupiga doria katika bahari ya Pembe ya Afrika, hali imezidi kuwa mbaya mwaka 2009 ya vitendo vya uharamia wa kuteka meli kushamiri.

Wiki iliyopita serikali ya mpito ya Somalia iliiomba jumuia ya Kimataifa kusaidia kuunda kikosi cha kitaifa cha ulinzi wa bahari katika jitahada za kupambana na uharamia na pia kuwalinda wavuvi kutokana na mashua za uvuvi za kigeni na halikadhalika kuzuia utupwaji wa taka za sumu katika pwani ya Somalia.


Source: BBC